Mwanasayansi wa Maabara wa Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila Bw. Jastus Silvester akimuhudumia Bi. Foibe Jackson kutoka Kanisa la Anglikana wilaya ya Ubungo ambaye ni mmoja wa vijana wa Kanisa la Anglikana ambao leo wamejitokeza kuchangia damu katika Hospitali ya Mloganzila.
Mwanasayansi wa Maabara Bw. Mbaruku Kisutu (kulia) akimsajili Bw. Fredrick Anderson (kushoto) kabla ya kuingia katika chumba cha uchangiaji damu.
Baadhi ya vijana kutoka Kanisa la Anglikana wilaya ya Ubungo ambao leo wamejitokeza kuchangia damu katika Hospitali ya Mloganzila.
……………….
Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila imetoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kujitolea katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuchangia damu wagonjwa ambao wanauhitaji wa damu ili kuokoa maisha yao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi MNH-Mloganzila Dkt. Lulu Sakafu wakati akizungumza kwa niaba ya Naibu Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Julieth Magandi katika zoezi la uchangiaji damu kutoka kwa vijana wa Kanisa la Anglikana wilaya ya Ubungo.
Dkt. Sakafu amesema mahitaji ya damu katika Hospitali ya Mloganzila ni chupa 40 kwa siku lakini damu inayokusanywa ni kati ya chupa 15 mpaka 20 na kusisitiza kuwa pamoja na hali hiyo hakuna mgonjwa anayekosa damu.
“Napenda kusisitiza kwamba pamoja na kukusanya chupa 20 za damu kwa siku, hakuna mgonjwa anayekosa damu katika Hospitali ya Mloganzila kwasababu tunasaidiana na wenzetu wa Muhimbili-Upanga, kituo cha damu salama pamoja na Hospitali za Tumbi na Mlandizi’’ amesema Dkt. Sakafu.
“Pia nachukua fursa hii kushukuru Kanisa la Anglikana kwa matendo ya huruma unapochangia damu unaokoa maisha ya watu, kwani makundi yenye uhitaji wa damu ni mengi ikiwemo mama wajawazito, watoto, wagonjwa wanaohiaji kufanyia upasuaji na majeruhi wa ajali’’ amefafanua Dk. Sakafu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Vijana Kanisa la Anglikana wilaya ya Ubungo Bw. Daniel Katumbi amesema kanisa hilo limekuwa na utaratibu wa kufanya matendo ya huruma kila mwaka kwa kutambua kuwa wapo watu wenye mahitaji mbalimbali hivyo ni wajibu wa kanisa kuwatambua na kutoa huduma.
Katika zoezi hilo takribani vijana 50 wamechangia damu.