Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Consolata Mushi wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya kufanyika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani
………………………..
NA MUSSA KHALID
Imeelezwa kuwa Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumwa na watu wengi duniani ambapo kwa sasa kina zaidi ya watu Milioni 200 duniani na kinafundishwa katika vyuo vikuu zaidi ya 58.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Consolata Mushi wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya kufanyika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yanatarajiwa kufanyika July,7 mwaka huu.
Bi.Consolata amesema kuwa hiyo inatokana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi,na Utamaduni (UNESCO) Nov,23 mwaka jana ambalo lilitangaza kuwa lugha ya Kiswahili imetambuliwa kama lugha rasmi miongoni mwake zikiwamo Kiingereza,Kifaransa,Kichini,Kirusi,Kispanyola na Kiarabu.
Aidha Bi,Consolata amesema kuwa hadi ya Kiswahili Duniani ni kubwa na hiyo ndio ambayo imesababisha kutengewa siku yake maalum.
‘Kihistoria tar 7/7 ya kila mwaka ni siku muhimu kwa watanzania kwani pia Muasisi wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alianza kutumia Kiswahili kama lugha ya kuwaunganisha watanzania katika harakati za kudai uhuru,Pili mwaka 2000 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza upya baada ya kuwa ulivunjika mwaka 1977 na tatu ni sabasaba ambayo ni maonyesho ya biashara kimataifa nchini’amesema Bi Consolata
Amesema serikali kupitia BAKITA imepanga mambo yatakayofanyika katika siku hiyo adhimu ya Kiswahili kuwa ni pamoja na kufanya makongamano ya ndani yatakayohusisha mada mbalimbali zinazohusu Kiswahili,siku maalum ya Utamaduni wa mswahili na kutafanyika mijadala inayohusisha wanafunzi wa Kiswahili katika ngazi vyuo vya kati na juu.
Vilevile amesema kuwa katika kuelekea siku hiyo kutakuwa na siku maalum ya wanafunzi wa ngazi ya shul za Msingi,Sekondari ambapo kutakuwa na makala ya kuelekeza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili pamoja na utamaduni wake,Kughani Mashairi,Nyimbo,Ngoma na sanaa mbalimbali za Kiswahili.
Ameendelea kusema kuwa kutambuliwa na kutengewa siku maalum kwa lugha ya Kiswahili kunamaanisha kuwa ni dhahiri shahiri Watanzania watafaidika kwa fursa za ajira,biashara na kutangaza utalii na utamaduni wa Mswahili.
Ametaja mafanikio ya Lugha ya Kiswahili kuwa mpaka sasa ni miongoniu mwa lugha rasmi katika Afrika hususani kwenye Bung la Afrika,Umoja wa Afrika,Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).