Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe,
akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu, kuhusu maamuzi ya Serikali katika utekelezaji wa madeni
yanayodaiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kwa wadaiwa sugu mjini
Dodoma.
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Elias Kwandikwa, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Sekta hiyo
kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa
Selemani Kakoso, akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano pamoja na Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Sekta ya Ujenzi mara
baada ya kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Sekta hiyo, mjini Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Viongozi na
Watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Taasisi zilizo chini
yake, wakiwa katika kikao kilichohusisha uwasilishaji taarifa ya utekelezaji wa
maazimio ya kamati hiyo, mjini Dodoma.
**************
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe,
amesisitiza kuwa Wizara kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) itaendelea
kuwaondoa wadaiwa sugu wa kodi ya pango za majengo na nyumba za watumishi wa umma, wabunge na baadhi ya Taasisi za Serikali lengo likiwa ni kuimarisha Wakala huo ili uweze kujiendesha wenyewe na hatimaye kuweza kukamilisha miradi mingine inayoitekeleza.
Alisisitiza hayo katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu
jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na mmoja wa wajumbe wa kamati
hiyo aliyetaka kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo.
Aliongeza kuwa uamuzi huo wa kuwaondoa wadaiwa sugu unazingatia taratibu
stahiki ambazo zinatambulika kisheria.
“Wizara imeamua kufanya hivi kwa mujibu wa sheria kwani Wakala unadai
wateja wake zaidi ya shilingi bilioni 20 hivyo tukiendelea kulimbikiza madeni
haya, Wakala utashindwa kujiendesha na hatimaye kufa kabisa” alifafanua Waziri
Kamwelwe.
Aidha, Waziri Kamwelwe, amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19
Wakala huo umefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 19 kutoka vyanzo
vyake vya ndani vya mapato na Wakala unatarajia kukusanya zaidi ya shilingi
bilioni 114 katika mwaka wa fedha 2019/20.
Ameendelea kueleza kuwa hadi kufikia Juni, 2019 Wakala umekamilisha baadhi
ya miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma
na ujenzi wa nyumba kwenye mradi wa kufufua umeme iliyopo Wilaya ya Rufiji
mkoani Pwani.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, wakati akiwasilisha taarifa ya sekta hiyo, Naibu
Waziri huyo aliielezea kamati hiyo kuwa Serikali inaendelea kulipa fidia kwa
wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege
hapa nchini na tayari bilioni 5.7 zimeshapokelewa Wizarani kwa ajili ya fidia ya
Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Selemani Kakoso,
ameishauri Wizara kupitia Wakala huo kuhakikisha inaondoa kero na malalamiko
ya wateja wake kwa kufanya maboresho ya nyumba zake.
Aliendelea kushauri kuwa Serikali iangalie namna ya kuwapatia Wakala mfuko
wa dharura kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyosimama hususani ile ambayo ipo
katika hatua ya kuiongezea Serikali gharama kubwa kwa kutoendelea kwa ujenzi
huo.
Kikao cha Kamati hiyo kimeshirikisha wajumbe mbalimbali ikiwemo Naibu
Waziri wa Sekta ya Ujenzi Elias Kwandikwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi
Mhandisi Atashasta Nditiye na kinaendelea kupokea taarifa ya utekelezaji ya Sekta
hiyo ambayo inatokana na maazimio ya vikao vya Bunge vilivyopita.