Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lililo chini ya Wizara ya Afya, Prof. Hamisi Malebo (katikati) akizungumza juu ya shughuli za Baraza hilo ikiwemo kupongeza Waganga walioshirikiana bega kwa bega kwenye mapambano ya ugonjwa wa UVIKO 19
SERIKALI kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lililo chini ya Wizara ya Afya limeshukuru wadau waliojisajiliwa na Baraza hilo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 tokea kuingia hapa nchini mwaka 2020.
Akitoa shukrani hiyo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo Prof. Hamisi Malebo alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa waganga hao wa tiba asili na tiba mbadala kwa namna walivyoshirikiana bega kwa bega na Serikali.
‘’Tunawashukuru kwa dhati na kuwapongeza waganga wa tiba asili na mbadala na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa UVIKO 19 tangu umeingia hapa nchini mwaka 2020.
Pia Wananchi kuiamini na kuitumia tiba asili ambayo ni urithi tulioachiwa na mababu zetu.
Aliongeza kuwa; Hii tiba ni huduma rasmi na Serikali iliona umuhimu na kutungia sheria ilikutambulika na kuendeleza huku ikiwataka waganga na wauza dawa na vituo vyote kusajiliwa na Baraza.’’ Alisema Prof. Malebo.
Katika hatua nyingine, alitoa rai kwa waganga wote waweze kujisajili iliwaweze kutambulika kisheria huku pia akitaka waganga hao kuchangamkia fursa za vibali vya kusafirisha dawa za ndani kwenda kwenye soko la dunia.
‘’Katika kuondoa kero na kutekeleza maagizo, kwa sasa baraza limeanza kutoa vibali vya kusafirisha dawa na malighafi za dawaa asili za Tanzania kusafirishwa nje ya Tanzania.
Hatua hii itakuza tiba asili ya Tanzania na tiba asili kwenye masoko mengine ya kimataifa ikiwemo kuongezea vipato wahusika na Serikali.’’ Alisema Prof. Malebo.
Katika suala la usajili, Prof. Malebo alisema kuwa hadi sasa tayari zaidi ya Waganga3000 wamesajiliwa hadi Desemba mwaka 2021.
‘’Mwaka 2010 na hadi kufikia Desemba 31, 2021 Baraza lilisajili jumla ya Waganga 3121.
Vikiwepo vituo 1094 na dawa 73 za asili ziliweza kusajiliwa na kutambulika rasmi na Baraza.’’ Alisema Prof Malebo.
Aidha, ametoa rai kuacha mara moja waganga wasiofuata sheria za Baraza hilo huku kwa wale ambao leseni zao zimeisha muda wake kuziuhisha tena;
‘’Kumekuwepo na waganga wasiofuata utaratibu na miongozo ya baraza. Wapo waganga wanaotoa huduma bila kujisajili lakini pia wanaotumia vibaya uganga wao ikiwemo kuweka picha za utupu na zisizo na maadili katika uganga wao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa mwanasheria mkuu, ofisi ya mwanasheria mkuu ambaye ni Mjumbe wa baraza hilo, Bi. Frida Mwera alisema kuwa baraza hilo linajiendesha kikanuni ambapo imewataka waganga wote kabla ya kuanza kazi zao lazima wapate kusajiliwa na endapo akikutwa na kosa basi atapata adhabu kali ikiwemo kifungo cha gerezani na faini.
‘’Tunasisitiza waganga wote wa kujisajili ndani ya baraza ilikuepuka makosa ya kisheria.
Pia mahakama inamamlaka ya kutoa amri ya kutaifishwa dawa ama kutupwa ama kuharibiwa kwa dawa husika zitakazokutwa kwa Mganga aliyeenda kinyume ambaye hajapata usajili wa Baraza.
Tiba asili na tiba ni huduma rasmi ambazo zilijumuishwa kwenye sera ya Afya tangu mwaka 1990, baada ya Serikali kuona umuhimu wa huduma hii ambayo bado inahitajika sana katika jamii yetu.
Mwaka 2002 Sheria namba 23 ilitungwa na Bunge na mwaka 2005 Baraza la Tiba asili na mbadala liliundwa rasmi kwa lengo la kusimamia, kudhibiti na kuendeleza tiba asili na tiba hapa nchini na kuwataka waganga,wauza dawa na vituo vyote kusajiliwa na Baraza.
Ambapo Serikali imeweza kuongeza juhudi mbalimbali ya uendelezaji wa tiba asili na tiba mbadala imejiwekea malengo ikiwemo masuala ya utafiti, uzalishaji na matumizi ya tiba asili katika mfumo wa afya.