Mwamuzi kutoka nchini Zambia Janny Sikazwe amezua balaa kwenye michuano ya AFCON inayoendelea kutimua vumbi huko Cameroon wakati wa mchezo wa kundi F kati ya Tunisia na Mali uliomalizika kwa Mali kuibuka na ushindi wa 1-0.
Maamuzi ya utata yaliyotolewa na refa huyo katika mchezo huo yamezua mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii na kuzua sintofahamu ya utimamu wa mwamuzi huyo kiafya hususani katika kipindi cha pili cha mchezo huyo.
Refa Janny awali alipuliza kimakosa kipyenga cha kumaliza mtanange huo dakika ya 85 tu kabla ya kupata shinikizo kutoka kwa wachezaji na Benchi la ufundi la Tunisia na kubatilisha uamuzi huo.
Hata hivyo mara tu baada ya kuruhusu mchezo kuendelea refa huyo akamuonesha kadi nyekundu iliyokuwa na utata mkubwa mshambuliaji wa Mali El Bilal Toure.
Kabla ya kuibua utata mwingine kwa kupuliza kipyenga cha kumaliza mchezo huo dakika ya 89 bila ya kuwa na sababu maalumu kitendo kilichowakera Tunisia.
Vikosi vya usalama vililazimika kuingia uwanjani kwa ajili ya kumlinda kutokana na wafanyakazi na benchi la timu ya Taifa ya Tunisia waliojawa na ghadhabu kutokana na utendaji wa mwamuzi huyo.
Ikumbukwe mwaka 2018 Novemba 20,CAF walimfungia mwamuzi huyo baada ya kubainika kupokea rushwa na kuharibu mchezo wa nusu fainali ya pili wa ligi ya mabingwa Afrika kati ya Espérance de Tunis ya Tunisia walioshinda 4–2 dhidi ya Primeiro de Agosto kutoka Angola.