Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma Neema Maghembe kulia,akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge jana ambapo ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa chini ya mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid 19 umefikia asilimia 7
Picha na Muhidin Amri.
***************************
Na Muhidin Amri,
Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Songea kwa kazi nzuri katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa yanayojengwa katika shule mbalimbali za sekondari.
Jenerali Ibuge ametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti, wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa chini ya mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 katika shule ya Sekondari Maposeni na Mpitimbi.
“Mkurugenzi na wataalam wako nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya,nimepita maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuangalia kazi ya ujenzi wa miradi hii ya Covid-19 lakini nyinyi mmenifurahisha sana”alisema Ibuge.
Alisema, licha ya majengo yake kufikia hatua nzuri ya utekelezaji wake,pia yamejengwa kwa ubora wa hali ya juu na kuzitaka Halmashauri nyingine za mkoa huo kwenda kujifunza namna ya utekelezaji wa miradi hiyo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea.
Alisema,ataendelea kusimamia fedha zinazoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo na hatokubali hata kidogo kuona baadhi ya miradi inajengwa chini ya kiwango.
Hata hivyo,amemuagiza Mhandisi wa ujenzi kufanya marekebisho madogo kwenye ngazi za kuingia darasani na ofisi za walimu ili watu wenye mahitaji maalum(walemavu) ili iwe rahisi nao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea Neema Maghembe alisema, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri hiyo imepokea jumla ya Sh. 500,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa wa vituo vya afya viwili vya Liganga na Kilagano ambapo kila kituo kimepatiwa Sh. 250,000,000.00.
Aidha alisema,Halmashauri imepokea Sh. 90,000,000.00 kujenga nyumba tatu za watumishi katika kituo cha afya Matimila ambapo ujenzi wake upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Akizungumzia ujenzi wa vyumba vya madarasa alisema, wamepokea Sh.380,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika vituo shikizi vya shule za msingi tano ambazo ni Jenister,Mhimbasi,Lihulu,Lunyele na Ligunga.
Pia alimueleza Mkuu wa mkoa kuwa,Halmashauri imepokea mgao wa Sh. 920,000,000.00 ambazo zimeanza kutumika kujenga vyumba 46 vya madarasa kwenye shule 16 za Sekondari.
Maghembe alisema,utekelezaji wa mkiradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali ambapo ujenzi wa vyumba viwili katika ya Mpitimbi upo katika hatua ya umaliziaji, na shule saba zenye jumla ya vyumba 17 tayari zimeezekwa bati pamoja na upigaji wa lipu ndani na nje.
Kwa mujibu wa Maghembe,kazi za ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule shikizi na shule za sekondari unaendelea vizuri na umefikia asilimia 70.