*************************
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
JAMII imehimizwa kupanda miti mbalimbali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani miti hususan ya asili inatajwa kuwa hatarini kutoweka .
Aidha kila mwananchi ,ameaswa kuwa mabalozi wa kulinda Mazingira na kutunza miti inayopandwa kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Akizungumza kwenye zoezi la upandaji miti katika shule ya Sekondari Pichandege, wakati Halmashauri ya mji wa Kibaha,ilipofanya maadhimisho ya siku ya uhuru kuelekea siku ya uhuru Desemba 9 ,ambapo inatimia Miaka 60 ya Uhuru na 59 Jamhuri ,Afisa Tarafa Kibaha , akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo , Anatory Mhango alisema ,miti ikikatwa ovyo kunaondoa uoto wa asili.
Alisema , Halmashauri hiyo, imejipanga kupanda miti 10,000 hadi kufikia mwezi March mwakani ili kukabiliana na Hali ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mhango aliiomba jamii kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kupanda Miche ya miti kwenye maeneo Yao, maeneo ya shule , Zahanati na vituo vya afya.
Diwani wa kata ya Pichandege,Karim Mtambo alielezea, miti ina faida kubwa kama itatunzwa ,miti inatunza Mazingira, miti hii shuleni ,italinda udongo kusiwepo na mmonyoko wa udongo na kuwapa vivuli wanafunzi na kupata maeneo ya kupumzika.
Alikemea kukata miti ovyo kwakuwa miti Ni rafiki kwani inatuletea hewa safi.
“Miti inayopandwa pia unatakiwa ilindwe kwa manufaa ya baadae ,watu waache kukata miti ovyo ,kwani kutoweka kwa miti kunasababisha mvua kutoweka na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi”alisema Mtambo.
Vilevile, William Daudi afisa Misitu Halmashauri ya Mji wa Kibaha, alisema Halmashauri imelenga kupanda Miche Cha miti zaidi ya 10,000 katika maadhimisho hayo na wanatarajia kupanda miti 542,000 kwa kushirikiana na Taasisi TFS, meneja wa Misitu Kibaha kupanda miti katika msimu wa mvua kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha.
Alieleza,katika zoezi hilo wamepanda miti 200 , shule ya Sekondari Pichandege kuunga mkono maadhimisho ya siku ya Uhuru.
Daudi aliipongeza shule hiyo kwa kuthamini umuhimu wa Mazingira ambapo wameshapanda miti 1,000,na kushauri Halmashauri na wilaya nyingine nchini kuiga mfano wa Halmashauri na shule hiyo .
Nae Mwalimu wa Mazingira Shule ya Sekondari Pichandege, Ndunguru alisema matarajio Yao Ni kupanda miti mingi na kuilinda .
Alifafanua,shule hiyo ina eneo la hekari 11.7 wanalotarajia kupanda miti na hadi sasa wamepanda miti 1,000 ikiwemo miti 980 ya vivuli na miti ya matunda 20.