Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete (kulia) akijadiliana jambo na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Andrea Pembe (kushoto) kwenye maafali hayo.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete akizungumza kwenye Mahafali hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo hicho Nijini Dar es Salaam.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete akiwatunuku wahitimu wa Shahada ya uzamivu (PhD) kwenye Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam, leo.
Wahitimu wanne walopata Shahada ya juu ya Uzamivu ya udaktari wa Falsafa (wa kwanza kushoto waliokaa viti vya mbele), ni Mourice Mbunde,(kulia) ni Mboka Jacob, (waliokaa viti vya nyuma), ni Baraka Samweli (kulia),na Zuhura Idd Kimera (kushoto).
Na: Mwandishi wetu, Dar
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete leo Disema 4,2021 ameongoza sherehe za Mahafali ya 15 ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS) yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho Jijini Dar es salaam.
Katika Mahafali hayo Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Mkuu wa Chuo hicho Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Alli Hassani Mwinyi ambapo aliweza kutunuku Shahada kwa wahitimu wa kada mbalimbali katika sekta ya Afya wakiwemo wahitimu wanne wa Stahada ya Uzamivu (PhD).
Akizungumza kabla ya kuwatunuku Shahada wahitimu hao, Rais Mstaafu Kikwete aliwapongeza wahitimu wote kwa hatua waliyofikia na kuwahimiza kwenda kufanyakazi kwa bidii na maarifa ili kuisaidia Serikali ambayo imewekeza fedha nyingi kwenye sekta hiyo kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za Afya.
“Nitoe rai kwenu ninyi wote mnaohitimu leo muende mkafanyekazi kwa bidii katika maeneo mbalimbali mtakayopangiwa na Serikali ili kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kuboresha huduma za Afya kwa kujenga miundombinu na kuhimarisha huduma za Afya” Amesema.
Aidha amebainisha kuwa kuna idadi ndogo ya wahitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika vyuo vikuu vya hapa nchini tofauti na nchi nyingine za Afrika mashariki nakwamba ameutaka uongozi wa chuo hicho kuwa na Programu maalum ya kuwasaidia wanafunzi wenye sifa na uwezo wapate fursa ya kuendelea na masomo ili kupata wataalamu wa kutosha kwenye vyuo na Taasisi za elimu ya juu hapa nchini.
“Nitoe rai kwenu kuweka mipango maalum itakayowawezesha wanafunzi wenye sifa kujiendeleza katika ngazi ya juu ili kuwa na wataalamu wengi watakaosaidia kupunguza tatizo la wataalamu kwenye Vyuo vyetu”
Na kuongeza kuwa” Nchi yetu bado tuna idadi ndogo ya wahitimu wa Shahada ya Uzamivu tofauti na nchi za majirani zetu katika afrika Mashariki ambao uzalisha wahitimu wengi wa PhD” Aliongeza Mhe: Kikwete huku akitolea mfano wa Kenya ambao walikuwa na idadi kubwa ya wahitimu 80 wakati wa uongozi wake.
Akizungumza kwenye Mahafali hayo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa
miongoni mwa mambo yaliyopo katika mpango mkakati wa Chuo hicho nikuongeza udahili wa wanafunzi, kuongeza ubora wa mafunzo na ufundishaji, kuwaongezea uwezo watafiti ili kuwa na ubora zaidi, kuboresha miundombinu ya kufundishia, kuboresha Maktaba pamoja na miundombinu ya TEHAMA.
“Pamoja
na Juhudi zote zinazofanywa na Chuo katika kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ya nchi iliyoainishwa katika sekta ya afya na elimu, ufanisi mkubwa zaidi unaweza kupatikana pale ambapo Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi kuliko ilivyo sasa” Amesema Dkt. Mwakyembe.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Andrea Pembe ameelezea mwenendo wa zoezi la udahili wanafanzi katika chuo hicho nakwamba kwa mwaka wa masomo 2021/2022 Chuo kimedahili wanafunzi 848 wa Shahada ya kwanza na wanafunzi 169 wa Stashahada katika fani mbalimbali za afya.
“Kwa mwaka huu wa masomo udahili wa masomo umeongezeka kwa asilimia nne (4%) ukilinganisha na udahili wa mwaka jana ambapo Chuo kilidahili wanafunzi 815 wa Shahada ya kwanza” Amesema Profesa Pembe.
Na kuongeza kuwa “Chuo bado kinaendeleza juhudi mbalimbali za kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kutosha katika Kampasi ya Mloganila na upatikanaji wa Rasilimali watu ya kutosha ili kuwezesha udahili wa
idadi kubwa ya wanafunzi” Ameongeza Profesa Pembe.