Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC akiongea na vyombo vya habari kwenye mapango ya Amboni Jijini Tanga kufuatia mgogoro baina ya wachimbaji wa madini wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini karibu na mapango hayo na mamlaka ya uhifadhi ya Ngorongoro inayohifadhi mapango hayo.
Sehemu ya mapango ya Amboni ambayo yanahifadhiwa na mamlaka ya Ngorongoro.
Sehemu ya Maafisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, waandishi wa habari pamoja na Maafisa kutoka mamlaka ya Ngorongoro wakiwa kwenye mapango ya Amboni.
******************
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC amesema shughuli za kibinadamu ni muhimu kufanyika kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji wa mazingira ili kuepuka madhara ya uharibifu wa mazingira yasijitokeze katika Taifa letu.
Dkt. Gwamaka ameyasema hayo alipofanya ziara katika hifadhi ya mapango ya Amboni Jijini Tanga alipokwenda kukagua uhifadhi wa mazingira katika mapango hayo.
“Kuna shughuli za uchimbaji wa madini kwa kutumia baruti karibu na mapango haya zinazopelekea mitetemo ambayo inasababisha kuleta nyufa zinazoruhusu maji kujaa kwenye mapango haya.
Dkt. Gwamaka ameongeza kuwa shughuli za uchimbaji wa madini karibu na mapango ya Amboni zinapingana na uhifadhi wa mazingira, lakini pamoja na hayo Waakazi wa eneo hilo wameshiriki kuyahifadhi mapango hayo kwakuwa wapo hapo toka mwaka 1934 hivyo NEMC itashirikiana na mamlaka husika yaani watu wa madini, mamlaka ya Ngorongoro na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga ili kupata suluhu ya tatizo hili mapema kabla mapango hayo hayajapotea lakini wakati huo huo na Wananchi wapate haki yao ya kuyahifadhi kwa muda wote huo.
Naye Bw. Thobias Mwesiga Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka NEMC amesema milipuko inayosababishwa na uchimbaji wa madini karibu na mapango ya Pangani ina athari kubwa kwasababu inaweza kusababisha nyufa kwenye mapango hatimaye yanaweza kupoteza uhalisia wake.
Bw. Mwesiga amesema ni muhimu kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kwani itasaidia kuepuka uharibifu wa mazingira.
Naye Bi. Luhuvilo Mwamila Mhandisi Muandamizi wa Mazingira kutoka
Ofisi ya Kanda ya Mashariki Kaskazini NEMC amesema ingawa mapango yamekuta kijiji lakini kuna umuhimu wa kuangalia athari za kimazingira zinazoweza kusababishwa na shughuli za wachimbaji wadogo wa madini wanaotumia milipuko karibu na mapango.
B. Luhuvilo ameongeza kwa kushauri kuwa mamlaka za madini (waliotoa leseni za uchimbaji), NEMC na Hifadhi ya Ngorongoro zikae pamoja pamoja kutatua changamoto hii.