Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Uwekezaji Mh. Angellah Kairuki (kushoto)
akisalimiana na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili alipowasili kwa
ajili ya kukabidhi msaada katika wodi ya watoto mwenye magonjwa ya
saratani.
Waziri Angellah Kairuki akicheza na watoto mara baada ya kuwasili
Muhimbili leo.
Mhe. Kairuki (kushoto) akikabidhi msaada wa vitanda 10, mashuka 100
pamoja na vifaa vya kupimia mapigo ya moyo katika wodi ya watoto.
Vitanda ambavyo Waziri Kairuki amekabidhi kwa wodi ya watoto katika
Hospitali ya Tafa Muhimbili.
*************
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Uwekezaji Mh. Angellah Kairuki leo ametoa msaada
wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 kwa wodi ya
watoto mwenye magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH).
Baadhi ya vifaa hivyo ni vitanda 10, mashuka 100 pamoja na vifaa vya kupimia
mapigo ya moyo ambavyo vyote vitatumika katika wodi ya watoto wenye saratani.
Mh. Kairuki amesema vifaa hivyo amevitoa yeye binafsi kwa kushirikiana na
wadau kutoka China ambao aliwaeleza lengo lake na wakaguswa kushirikiana
naye katika kufanikisha hilo.
“Baada ya kuwasiliana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kujua mahitaji ya wodi
hii, niliwatafuta wafadhili wakaniunga mkono lakini sitaishia hapa nitaendelea
kutafuta wadau wengine ili waendelee kuwasaidia watoto hawa wanaosumbuliwa
na maradhi ya saratani’’amesema Mh. Kairuki.
Waziri Kairuki pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza watoa huduma wa
Muhimbili kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia watoto wenye
Saratani ambao wanapata huduma hospitalini hapo.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Prof. Lawrence Museru,
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Sista Zuhura Mawona amesema
msaada huo umekuja wakati muafaka kwakuwa wodi ya watoto wenye Saratani ina vitanda 68 ambavyo wakati mwingine havitoshelezi mahitaji.
“Msaada huu utatumika kama ilivyokusudiwa na mahitaji mengine uliotupatia
ikiwemo sabuni tutawagawia walengwa’’ amesema Sista Mawona.
Kwa Upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MNH Bw. Aminiel
Aligaesha amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili ipo katika hatua za mwisho za
za maandalizi ya kutoa huduma ya kupandikiza Uloto (Bone Marrow Transplant)
ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa
wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi na kugharimu fedha nyingi.
“Maandalizi tumeshafanya tulipeleka wataalam 11 nchini India kwa ajili ya
kujifunza kwa vitendo jinsi ya kufanya upandikizaji wa uloto na wataalam hawa
tayari wamerejea”. Amesema Bw.Aligaesha.