Home Mchanganyiko Mkoa wa Tabora wachangia damu majeruhi wa ajali ya moto

Mkoa wa Tabora wachangia damu majeruhi wa ajali ya moto

0

Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili
(Katikati), Bw.Aminiel Aligaesha akizungumza na waandishi wa habari wakati wa
kupokea msaada wa damu kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora. Kushoto ni
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi Muhimbili Dkt.Praxeda Ogweyo na
kulia ni Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dkt. Magdalena Lyimo.

Dkt. Magdalena Lyimo akiongea na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi
msaada wa Damu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mh. Agrey Mwanri.

Dkt Magdalena Lyimo (kulia)akimkabidhi Dkt. Praxeda Ogweyo (kushoto), unit
100 za damu kwa niaba ya Mh.Mwanri.

****************

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), leo imepokea msaada wa damu unit 100
kutoka kwa Mkuu wa mkoa wa Tabora Mh. Agrey Mwanri kwa lengo la kusaidia
majeruhi wa ajali ya moto wanaoendelea kupatiwa matibabu Muhimbili.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mh. Mwanri, Meneja wa Mpango wa Taifa
wa Damu Salama Dk.Magdalena Lyimo amesema mkuu wa mkoa wa mkoa wa
Tabora ameguswa na ajali ya moto iliyotokea Agosti 10 mwaka huu mkoani
Morogoro iliyosabaisha vifo na majeruhi.

“Mh. Mwanri ameguswa na tatizo lililotokea mkoani Morogoro hivyo ameona ni
vema akahamasisha wananchi mkoani kwake kuchangia damu ili kuwasaidia
majeruhi wa moto na zoezi hili ni endelevu wataendelea kuchangia damu kadri
inavyowezekana.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
ya Umma Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) Bw. Aminiel Aligaesha amesema
hospitali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na serikali, watu pamoja na
makundi mbalimbali katika kusaidia majeruhi hao.

“Nawashukuru sana wakuu wa mikoa ikiwemo mkuu wa mkoa wa Tabora,
Morogoro na wote ambao wanaendelea kuhamasisha uchangiaji wa damu na kutoa misaada mbalimbali ‘’amesema Bw.Aligaesha

Kuhusu hali za majeruhi Bw. Aligaesha amesema kwa sasa majeruhi 20 kati ya 46
waliopokelewa wanaendelea kupatiwa matibabu kama inavyostahili ambapo
majeruhi wote wamehamishiwa katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) kwa ajili
ya ufuatiliaji wa karibu wa afya zao.