Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Beatus Kinyaiya, akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wanahisa wa Benki ya Biashara Mkombozi uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Thomas Enock na Kaimu Mwenyekiti wa bodi, Profesa Marcellina Chijoriga.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara Mkombozi, Thomas Enock, akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Kumi wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Beatus Kinyaiya na Mwenyekiti wa bodi, Profesa Marcellina Chijoriga.
Viongozi mbalimbali wakiwa meza kuu.
Wanahisa wakiwa kwenye mkutano huo.
Wanahisa wakijisajil kabla ya kuanza kwa mkutano huo
Mmoja wa Wanahisa akiuliza swali kwenye mkutano huo
Mwanahisa akichangia jambo kwenye mkutano huo
Na Dotto Mwaibale
MTAJI wa Benki ya Biashara Mkombozi umeongezeka kutoka shilingi za kitanzania bilioni 6.01 mwaka 2009 na kufikia shilingi za kitanzania bilioni 20.62 mwaka 2018.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Profesa Marcellina Chijoriga wakati akitoa taarifa kwenye mkutano mkuu wa kumi wa wanahisa
wa benki hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
” Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tangu kuanzishwa kwa benki yetu mwaka 2009 tumeshuhudia ukuaji wake kutoka hadhi ya benki ndogo mpaka kufikia benki ya hadhi ya kati kwa mantiki ya rasilimali, amana za wateja, shughuli za uendeshaji na faida” alisema Chijoriga.
Alisema mpaka sasa benki hiyo imeweza kufungua matawi 10, manne katika mkoa wa Dar es Salaam, moja katika mikoa ya Morogoro, Moshi, Mwanza, Kagera na hivi karibuni Iringa na Dodoma.
Aliongeza kuwa rasilimali za benki hiyo zimekua kutoka shilingi za kitanzania bilioni 8.69 mwaka 2009 na kufikia shilingi za kitanzania bilioni 178.82 mwaka 2018.
Alisema Amana za wateja nazo zimeongezeka kutoka shilingi za kitanzania bilioni 2.19 mwaka 2009 na kufikia shilingi za kitanzania bilioni 136.47 mwaka 2018 huku mikopo ikikua kutoka shilingi bilioni 37 mwaka 2009 na kufikia shilingi bilioni 99.04 mwaka 2018.
Alisema benki hiyo imefanikiwa kulipa gawio kwa wanahisa la thamani ya shilingi za kitanzania bilioni 0.41 mwaka 2016 na shilingi bilioni 0.52 mwaka 2017.
Akitaja mafanikio ya benki hiyo kwa mwaka 2018 alisema licha ya matatizo ya kiuchumi na mazingira ya soko benki hiyo iliweza kupata faida baada ya kulipa kodi ya shilingi za kitanzania milioni 806.04 na kuwa changamoto kubwa waliyokuwa nayo ilikuwa ni kuanza kwa matumizi ya Kanuni namba 9 ya Kanuni za Kimataifa za Uwasilishaji wa Taarifa za Fedha inayojulikana kitaalamu kama Internatipnal Reporting Standard (IFRS 9)
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya ambaye ni mmoja wa Wakurugenzi wa benki hiyo aliwaomba wanahisa wa benki hiyo kwa kipindi hiki kutochukua hisa zao kwani hali ya soko duniani sio nzuri hivyo wasubiri hali itakapo kuwa nzuri ndipo wachukue kwa faida kubwa.