Ujumbe wa Tanzania katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Uchumi na Uwekezaji wa Kampuni ya Sario ya Slovakia, Egon Zorad
Asteria Muhozya na Abubakari Kafumba, UAE
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Musa Budeba ameishawishi Slovakia kuwekeza Tanzania kwenye uchimbaji au ununuzi wa Madini ya Viwandani yanayotumika katika kutengeneza vifaa vya teknolojia mbalimbali yakiwemo magari.
Dkt. Budeba amemweleza Mkurugenzi wa Uchumi na Uwekezaji wa Kampuni ya Sario inayomilikiwa na Serikali ya nchi hiyo Bw. Egon Zorad, kuhusu uwepo madini hayo ambayo ni malighafi katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani.
‘’Tumeona Slovakia imepiga hatua katika masuala ya teknolojia ambapo wanatengeneza magari yanayotumia haidrojeni na tumeona wametengeneza mifano ya ndege. Kwetu sisi kama sekta ni fursa kuwavutia waje kuwekeza kwetu kwa ajili ya kupata malighafi ya kutengeneza bidhaa zao kwa sababu vitu vyote tulivyoviona vinahitaji malighafi zinazotokana na madini kama nickel, copper, rare earth elements, graphite na mengine ambayo yote yapo kwetu,’’ amesema Dkt. Budeba.
Ametoa kauli hiyo wakati wa kikao na mwakilishi huyo aliyefika katika banda la Tanzania baada ya wataalam wa Tanzania kutembelea banda la nchi hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Expo 2020 Dubai, ambapo walipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na nchi ya Slovakia likiwemo gari linalotumia hydrojeni.
Kwa mujibu wa Zorad, gari hilo ambalo limetengenezwa kwa takriban miaka mitatu, limetengenezwa na Vyuo Vikuu vya nchini humo kwa kushirikiana na Serikali na kampuni binafsi. Wataalam wa watanzania baada ya kutembelea banda hilo walifahamishwa kuhusu namna nchi hiyo inavyojaribu kukuza teknolojia zake na kuhamia katika mifumo mingine ya kiteknolojia ikiwemo matumizi ya magari yanayotumia umeme.
Aidha, Dkt. Budeba amemuhakikishia mwakilishi huyo kuhusu upatikanaji wa rasilimali za kutosha yakiwemo mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara yaliyopo nchini ikiwemo hali ya usalama, na uwepo wa miundombinu ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu huku pia, akieleza nia ya Tanzania kuunganishwa na wawekezaji wengine wakubwa kutoka Slovakia.
Pia, mbali na kuchimba na kununua madini, Dkt. Budeba amemshawishi kuhusu kufikiria namna Slovakia inavyoweza kuanzisha kampuni ya uundaji magari nchini Tanzania kutokana uhakika wa upatikanaji wa rasilimali ambazo zitahitajika katika uundaji bidhaa hizo. Vilevile, Dkt. Budeba amemuhakikishia kuwa, tayari Tanzania ina kanzidata yenye taarifa za kutosha kuhusu uwepo wa madini hayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Sario, Bw. Zorad ameshukuru kukutana na Wizara na kufahamishwa kuhusu uwepo wa rasilimali hizo na kutaka kupatiwa taarifa za kutosha kuhusu masuala muhimu ya uwekezaji na biashara ya madini Tanzania ili pia kampuni hiyo iweze kuiunganisha Tanzania na kampuni nyingine zilizoko Slovakia.
‘’Nataka sana Tanzania kuwa moja ya nchi tutakayoshirikiana nayo kwenye biashara na vyuo vyetu. Tumeelezwa kuwa nchi yenu iko kwenye nafasi nzuri kibiashara katika masuala ya madini. Slovakia tunaandaa mkutano wa wawekezaji na tunatarajia kualika angalau nchi moja kutoka Afrika na haina shaka itakuwa Tanzania,’’ amesema Zorad.
Mbali na masuala yanayohusu madini, pia, mwakilishi huyo wa Kampuni ya Sario, ameelezea nia ya Slovakia kutaka ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania hususan kwenye masuala ya utafiti.
Aidha, Dkt. Budeba na maafisa wengine wa Wizara ya Madini walifanya mkutano kwa njia ya mtandao na mwekezaji kutoka China aliyetaka kuwekeza kwa kushirikiana Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). Aidha Dkt. Budeba alimuunganisha mwekezaji huyo na Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO kwa hatua zaidi.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye Maonesha ya Expo 2020 Dubai, Bi. Getrude Ng’weshemi ameendelea kusisitiza ushiriki wa uhakika kama huu kwa sekta nyingine ambazo zinatarajiwa kushiriki katika maonesho haya ili kuhakikisha Tanzania inatumia vilivyo fursa zilizopo Dubai na kwingine duniani kupitia maonesho hayo.