Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza na waandishi wa habari leo November 8,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya wizara yake kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.
Waandishi wa habari wakifatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,(hayupo pichani) wakati akitoa taarifa ya wizara yake kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru kwa waandishi wa habari leo November 8,2021 jijini Dodoma.
…………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
KATIKA kipindi cha miaka 60 ya uhuru Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imewezesha wanawake kiuchumi,imeimarisha mifumo ya kupambana na kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake na Watoto na uwepo wa Sera, Sheria, Miongozo na mifumo ya kushughulikia masuala ya watoto.
Hayo yameelezwa leo Novemba 8,2021 Jijini Dodoma na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk.Doroth Gwajima wakati akieleza mafanikio ya Wizara hiyo kwa miaka 60 ya uhuru, amesema Serikali katika kipindi cha miaka 60 imewezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi.
“Ikiwemo kuwezesha nyenzo mbalimbali ikijumuisha kutoa mikopo isiyo na riba inayotokana na kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa,Mfuko waMaendeleo wa Wanawake, Dirisha la mikopo kwa wanawake kupitia Benki ya Wanawake na sasa Benki ya Posta, VICOBA, SACCOS,”amesema Dk.Gwajima
Pia amesema Serikali imeimarisha mifumo ya kupambana na kuzuia vitendo vya ukatili wa wanawake na Watoto kwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto yaani MTAKUWWA (2017/18 2021/22).
“Jitihada hizi zimewezesha kamati 18,186 mpaka sasa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa. Aidha, yameanzishwa Madawati ya Jinsia na Watoto 420 katika vituo vya Polisi, Madawati ya Jinsia 153 katika Jeshi la Magereza na Dawati katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kupambana na vitendo vya rushwa ya ngono kupitia Kampeni ya “Vunja Ukimya,”amesema.
Amesema baada ya Uhuru Serikali imejielekeza kwenye kuimarisha ustawi wa watoto ambapo, katika miaka ya mwanzo ya 1970 Wizara ilikuwa inaratibu na kusimamia upatikanaji wa haki na ulinzi wa mtoto kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
“Ili kuimarisha upatikanaji wa haki, maendeleo na ustawi wa mtoto, Serikali imeongeza wigo wa kutekeleza masuala ya watoto kwa kuridhia na kusaini mikataba ya kikanda na kimataifa,”amesema.
Vilevile,amesema baada ya uhuru, Serikali imepanua wigo wa majukwaa ya watoto katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo, katika kipindi cha mwanzo cha Uhuru wa Tanzania Bara, jukwaa pekee la watoto la kujadili masuala yanayowahusu na kufikisha ujumbe ilikuwa ni kupitia shule ikijumuisha majukwaa kama chipukizi.
Amesema Mfumo huo ulijumuisha watoto wale tu waliopo shule na kuwaacha watoto wasiokuwa shule na hivyo kutokutoa fursa sawa ya kushirikisha watoto wote.
Waziri Gwajima amesema mara baada ya Uhuru, Serikali ilihakikisha uwepo wa Sera, Sheria, Miongozo na mifumo ya kushughulikia masuala ya watoto ili kuimarisha mifumo ya kusimamia haki, ulinzi na ustawi wa watoto na kuwakinga dhidi ya ukatili wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia.
“Sera ya kwanza ya Maendeleo ya Mtoto iliandaliwa mwaka 1996 na kurejewa 2008 ambayo imeainisha haki tano za msingi kwa watoto; haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushiriki na haki ya kutobaguliwa,”amesema.
Vilevile,amesema Serikali imesajili jumla ya vituo 2,133 vya kulelea watoto wadogo mchana kwa ajili ya kutoa huduma za malezi na uchangamshi wa awali.
Aidha ili kukabiliana na changamoto za afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe Wizara iliratibu uandaaji na inasimamia utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe (2021/22 – 2024/25).
“Lengo likiwa kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana balehe wenye umri wa 10-19 katika ya maeneo ya VVU/UKIMWI, mimba za utotoni, ukatili, lishe bora, kuendelea kuwa shuleni na kujengewa ujuzi ili kupata fursa za kiuchumi,”amesema.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya makao ya watoto, Serikali inaratibu na kusimamia jumla ya makao ya watoto 239 ikilinganishwa na makao moja yaliyokuwepo mwaka 1960.
Amesema, Serikali kwa kushirikiana na shirika la ABBOT FUND imejenga Makao ya Watoto katika Eneo la Kikombo Mkoani Dodoma ambayo yalizinduliwa na Mhe. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema ushiriki wa wazee katika masuala mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo umeimarika baada ya Serikali kuweka utaratibu wa kuwa na Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote, ambayo yameanzishwa kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003.
Amesema Mabaraza 26 yameundwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na kufanya Mabaraza kufikia 20,748.
Amesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali kwa kutunga Sheria Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo ndiyo ilianza kuweka Taratibu za uratibu na usajili wa Mashirika hayo.
Aidha, katika kuimarisha utoaji wa huduma za usajili na uratibu Serikali imefanikiwa kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NIS) kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kuleta ufanisi na tija katika uratibu wa Mashirika hayo.
Kwa upande wa Afya Dk.Gwajima amesema kuwa ni idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote imeongezeka hadi kufikia vituo 8,537 ikilinganishwa na vituo 1,343 Mwaka 1960.
Amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 84.26 ambapo kati ya vituo hivyo, Serikali inamiliki asilimia 64, Mashirika ya dini asilimia 9 na vituo binafsi asilimia 27.
Amesema mtandao wa vituo vya huduma za afya umepanuka na kusogea karibu zaidi na wananchi ambapo zahanati ni 7,242 vituo vya afya 926 na Hospitali za Wilaya ni 178, Hospitali zingine ni 151.
Aidha, hospitali za kibingwa ngazi ya mikoa ni (28), ngazi ya Kanda Sita (6), hospitali za ubingwa maalumu ni Tano (5) na hospitali ya taifa ni moja (MNH).
Amesema vituo vyote hivyo vina jumla ya vitanda 90,488 ikiwa ni sawa na ongezeko la vitanda 71,656 sawa na asilimia 79.18.
“Kwa sasa uwiano wa vituo kwa idadi ya watu ni kituo kimoja kwa watu 6,751.5 (1: 6,751.5) tofauti na 1:40000-50000 kabla ya uhuru. Hivyo, Tanzania imefikia malengo ya umoja wa mataifa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa kuzingatia idadi ya watu na jiografia,”amesema.
Aidha, uwiano wa vitanda kwa idadi ya watu ni kitanda kimoja kwa watu 637 (1:637) ukilinganisha na 1:1000 kabla ya uhuru amedai mwaka 2020 uwiano wa wagonjwa kwa vitanda umekuwa kitanda kimoja kwa watu 19 (1:19).
Amesema idadi ya watumishi na wigo wa kada za wataalamu kwenye vituo vya huduma umepanuka kiasi kwamba hivi sasa vituo vya afya vinafanya hadi huduma za upasuaji mkubwa ambao awali ulikuwa haufanyiki.
“Idadi ya wataalamu wa baadhi ya kada mbalimbali za msingi kwenye afya waliosajiliwa imeongezeka hadi kufikia zaidi takribani 71,365 na usajili unaendelea kila siku.
“Hawa ni baadhi tu ya kada zinazojumuisha madaktari bingwa, wa kawaida, wauguzi, wataalamu wa maabara, mionzi, wafamasia na mionzi. Kabla ya uhuru wote hawa kwa ujumla walikuwa 435 tu. Hii ni hatua kubwa sana,”amesema.
Waziri Gwajima amesema hadi kufikia Juni, 2021 huduma za chanjo zimepanuka na kuimarika na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotekeleza kwa ufanisi eneo hili hususan chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja (1) huku utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 101.
Aidha, kila kituo cha huduma za afya kina huduma ya chanjo kwa ajili ya Kinga ya ugonjwa wa Polio (OPV3), PENTA-3 kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda (tetanus), homa ya ini na homa ya uti wa mgongo na chanjo ya Surua/ rubella.
Amesema idadi ya Kliniki za afya ya uzazi imeongezeka na sera ni kuwa katika kila kituo cha huduma za afya kuwe na huduma za afya ya uzazi na mtoto.
“Mifumo ya uongozi na uendeshaji wa vituo vya huduma za afya imeboreshwa kiasi kwamba wananchi nao ni sehemu ya bodi za ushauri, uendeshaji na kamati za ushauri na uendeshaji kuanzia hospitali za kitaifa hadi zahanati,”amesema.
Amesema hadi kufikia Juni, 2021, Mamlaka ilikuwa imesajili jumla ya viwanda vya ndani 36, ambapo 11 vya dawa, viwanda 14 vya vifaa tiba na 11 vya gesi tiba vinavyofanya kazi ukilinganisha na kiwanda kimoja cha dawa kilichokuwa kimesajiliwa wakati wa Uhuru mwaka 1961.
Amesema kuwa mafanikio mengine ni kuongezeka kwa umri wa kuishi wa mtanzania toka miaka 36 mwaka 1961 hadi miaka 66 mwaka 2020 ambayo inaashiria kuimarika kwa mifumo ya utoaji huduma za afya nchini.
“Hili ni ongezeko la mara mbili kwenye umri wa kuishi mtanzania,”amesema.