Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai kushoto akiongozana na Katibu mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya uvuvi Dk. Rashid Tamatama kushoto na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Patrick Boisafi katikati wakati akitembelea mabanda mbalimbali ya wadau wa Kilimo mara baada ya kuzindua maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Mandela eneo la Pasua mjini Moshi mkoani humo leo Jumanne Oktoba 12,2021. kilele cha maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa Lishe na Maisha Bora” kitakuwa Jumapili Oktoba 17,2021
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akipata maelezo kutoka kwa Anjelina Kimario mjasiriamali wa kilimo kutoka kikundi cha Kitarasa wilayani Rombo wakati alipotembelea banda hilo kujionea shughuli za kikundi hicho katika kilimo kushoto na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Patrick Boisafi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai na viongozi mbalimbali wakishiriki akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya wiki ya Chakula Duniani yanayofanyika mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Mandela eneo la Pasua mjini Moshi.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akizungumza wakati akizindua maadhimisho hayo leo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel.
Mkuu wa Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro Bw. Thompson Mwang’onda akimkaribisha Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai ili kuzungumza na washiriki wa maadhimisho hayo, Kushoto ni Katibu mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya uvuvi Dk. Rashid Tamatama
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Patrick Boisafi akizungumza katika uzinduzi huo kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai.
Mbunge wa jimbo la Moshi mjini Priscus Tarimo akichangia jambo wakati alipozungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo ya siku ya Chakula Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Mandelea Pasua mjini Moshi.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Uchumi inayomilikiwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini wakiwa katika banda lao tayari kwa kushiriki maadhimisho hayo ya siku ya Chakula Duniani.
Picha zikionesha mabanda mbalimbali yanayoonesha vyakula mbalimbali za zana za kilimo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akipata maelezo ya mashine ya kufyatuliamatofali wakati alipotembelea katika banda la zana za kilimo la kampuni ya Poly Machinery Co. Limited ya Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akipata maelezo ya mashine za kilimo wakati alipotembelea katika banda la zana za kilimo la kampuni ya Poly Machinery Co. Limited ya Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya, Edward Mpogolo Mkuu wa wilaya ya Same, Thopmson Mwang’onda Mkuu wa wilaya ya Siha na Mkuu wa wilaya ya Rombo Kanali Maiga wakiwakatika picha ya pamoja katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akisalimiana na wakuu za Mwanga, Mhe. Abdallah Mwaipaya, Edward Mpogolo Mkuu wa wilaya ya Same, Thopmson Mwang’onda Mkuu wa wilaya ya Siha na Mkuu wa wilaya ya Rombo Kanali Maiga waki alipowasili katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akisalimiana na wawakilishi wa shirika la Chakula Duniani (FAO) Tanzania wakati alipowasili katika uzinduzi wa maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akisalimiana na mmoja wa maafisa wa wizara ya kilimo Bi. Victoria Shirima alipowasili katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kuzindua maadhimisho hayo.
………………………………………………….
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Ndugu Steven Kagaigai amewaasa wakulima kutunza mazao kwa kufuata maelekezo sahihi kama yanavyotolewa na wataalam ili kuhakikisha chakula hakipotei bali kinatunzwa na ziada kuuzwa katika Soko la ndani na nje na kusaidia kuongeza kipato chenu.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro katika msimu wa 2020/2021 ulizalisha tani 1,248,299 sawa na 88.5% ya malengo. Uzalishaji huu unajumuisha tani 353,625 za mazao ya nafaka, tani 117,319 za mazao ya mizizi, tani 719,830 za ndizi na tani 57,525.
Steven Kagaigai ameyasema hayo wakati akizindua maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani leo kwenye viwanja vya Mandela eneo la Pasua mjini Moshi ambapo Taasisi na Mashirika mbalimbali ya serikali, Kimataifa ya yasiyokuwa ya kiserikali yanayojishughulisha na masuala ya kilimo yanashiriki katika maadhimisho hayo.
Aidha, ameongeza kuwa mahitaji ya chakula kimkoa ni tani 473,777 wanga na tani 47,378 za protini (mikunde). Uzalishaji halisi wa mazao ya wanga ni tani 514,567 na uzalishaji wa mazao ya mikunde ni tani 57,525. Kimkoa, Kilimanjaro kuna ziada ya chakula tani 40,790 za wanga na tani 10,147 za mikunde (protini).
Akizungumzia Sekta ya Mifugo, amesema kipindi cha mwaka 2020/2021 uzalishaji wa maziwa umefikia lita bilioni 3.1 ukilinganisha na lita bilioni 3.01 zilizozalishwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020.
“Ongezeko la uzalishaji huu limetokana na ongezeko la ngombe na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini. ambapo Pia uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kufikia tani 738,166 katika kipindi cha mwaka 2020/2021 tofauti na tani 701,679.1 zilizozalishwa mwaka 2019/2020.
Aidha, amefafanua kuwa pamoja na ongezeko hilo la uzalishaji, bado ulaji wa nyama na unywaji maziwa nchini sio wa kuridhisha.
Kiwango cha ulaji wa nyama Nchini kwa mtu kwa mwaka ni kilo 15, kiwango hiki kipo chini ukilinganisha na kiasi kinachopendekezwa cha kilo 50, kwa mtu kwa mwaka kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
Ameongeza kuwa kiwango cha unywaji wa maziwa nchini kwa mtu kwa mwaka ni takribani lita 55, kiwango hiki kipo chini ukilinganisha na kiasi kinachopendekezwa cha lita 200, kwa mtu kwa mwaka. Hivyo, niendelee kutoa rai kwa wananchi kuongeza ulaji wa nyama na unywaji wa maziwa ili tuweze kufikia viwango vinavyopendekezwa kwa lishe bora ya Watanzania.
Pia uzalishaji wa mayai umeongezeka nchini kutoka mayai bilioni 3.58 mwaka 2019/2020 hadi bilioni 4.5 mwaka 2020/2021 sawa na ongezeko la asilimia 26 ambapo ongezeko hili limesababishwa na kuongezeka kwa vituo vya kutotoleshea vifaranga vya kuku kutoka 26 mwaka 2019/2020 hadi 28 mwaka 2020/2021 na wananchi kuhamasika kufuga kuku kujikomboa kiuchumi na kuwa na uhakika wa chakula.
Ulaji wa mayai nchini kwa mtu kwa mwaka ni mayai 106 kiwango hiki kipo chini ukilinganisha na kiasi pendekezwa ambacho ni mayai 300 kwa mtu kwa mwaka.
Amesema katika sekta ya Uvuvi nayo ina mchango mkubwa katika kuwapa wananchi ajira, lishe bora, kipato na fedha za kigeni. Katika mwaka 2020/2021, Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.71 katika pato la Taifa na imetoa ajira kwa Watanzania takribani milioni 4.5.
Aidha, Sekta hii inachangia takribani asilimia 30 ya protini katika lishe inayotokana na wanyama. Uzalishaji wa mazao ya Uvuvi Kitaifa kwa mwaka uliopita 2020/2021 ulikuwa tani 473,592.24 na ulaji wa samaki kwa mtu ulifikia kilo 8.5 kiasi ambacho ni chini ya kiwango kinachoshauriwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) cha kilo 20.5.
Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, uvuvi unafanyika kupitia Bwawa la Nyumba ya Mungu Pamoja na mabwawa madogo madogo yapatayo 918 yanayomilikiwa na watu binafsi na Taasisi. Uzalishaji wa Samaki kimkoa kwa mwaka ni wastani wa tani 358 za Samaki.
Katika mwaka 2020/2021 Wizara imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji ambapo idadi ya wakuzaji viumbe maji (Wafugaji wa samaki) imeongezeka kutoka 28,009 mwaka 2019/2020 hadi 30,064 mwaka 2020/2021.
Kagaigai ameongeza kuwa idadi ya mabwawa imeongezeka kutoka 27,979 mwaka 2019/2020 hadi kufikia 30,032 mwaka 2020/2021 na vizimba vimeongezeka kutoka 431 mwaka 2019/2020 hadi 473.
Aidha, uzalishaji wa mazao ya Viumbe Maji hadi sasa umefikia tani 20,355.2. Ongezeko hili linaongeza upatikanaji wa Mazao ya Samaki katika Jamii yetu ili kuongeza ulaji wa samaki na kufikia Ulaji unaoshauriwa kitaalamu wa takribani Kilo 25 kwa kila mtu kwa mwaka.
Tumekusanyika hapa kwa ajili ya kuzindua maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo kauli mbiu yake ni “Zingatia uzalishaji na mazingira endelevu kwa lishe na mazingira bora,”.Amesema Kagaigai.
Kwa kuzingatia kauli mbiu hii na kwa kushirikiana na wadau Serikali imedhamiria kutatua changamoto za lishe kwa kuendelea kutekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe. Serikali kwa kupitia Wizara ya Kilimo na Wadau wa Lishe Nchini imeandaa mwongozo maalum kuhusu vyakula vilivyorutubishwa kibailojia (Biofortification Guidelines) ambao unategemea kuzinduliwa hivi karibuni kupunguza tatizo la lishe.
Hali ya Lishe Nchini si ya kuridhisha sana kutokana na takwimu kuonesha viwango vya juu ya utapiamlo hasa katika Mikoa inayozalisha vyakula kwa wingi.
Serikali imeendelea na juhudi za kuhakikisha hali ya utapiamlo Nchini inapungua kupitia mikakati na programu za kitaifa zinazoratibiwa na Ofisi ya Rais, Wizara za Kisekta na Wadau wa Maendeleo.
Kila mwaka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) huchagua kaulimbiu ambayo huwa inatoa dira ya kuhamasisha wadau wote wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuchangia katika kuhakikisha kila mtu anawezeshwa kupata chakula bora na cha kutosha wakati wote wa maisha yake. Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema ”Zingatia Uzalishaji na Mazingira Endelevu kwa Lishe na Maisha Bora.”
Maadhimisho haya ambayo yamezinduliwa rasmi kitaifa leo tarehe 12 Oktoba, 2021 mjini Moshi mkoani Kilimanjaro yatafikia kilele chake tarehe 17 Oktoba, 2021 hapa hapa katika Uwanja wa Mandela – Pasua katika Manispaa ya Moshi.