……………………………………………………………………
Na WAMJW-Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema zaidi ya watu 850,000 wameshapata chanjo ya UVIKO-19 mpaka kufikia Oktoba 9 2021 nchini kote.
Prof. Makubi amesema hayo leo Jumapili wakati akihamasisha waumini wa kanisa katoliki jimbo kuu Katoliki Dodoma ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya jamii harakishi na shirikishi inayoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Prof. Makubi amesema kupitia kampeni hiyo watu wengi wameelimishwa na kupata uelewa wa chanjo na kuondoa zile sintofahamu ambazo zilikua zinaleta hofu katika jamii na kupelekea wananchi wengi kupata hofu ya kwenda kuchanja.
Akihutubia waumini kanisani, Prof. Makubi amesema chanjo za UVIKO-19 aina ya Jensen na Sinopharm zilizoletwa nchini ni salama kwani zimethibitishwa na wataalam wa hapa nchini Pamoja na Shirika la afya duniani (WHO) hivyo amewataka wananchi kupuuza uzushi unaosambaa kuhusu madhara ya chanjo hizo na badala yake waende kuchanjwa ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza endapo mtu atapata maambukizi.
“Huenda kufikia Jumatano ya wiki ijayo chanjo zile chanjo milioni moja za Jensen zitakua zimeisha lakini Serikali imeshaleta chanjo nyingine za Sinopharm kutoka China na zimeshasambazwa kwenye vituo hivyo nawaomba wananchi kujitokeza kupata chanjo hizo ili kujikinga na madhara ya virusi vya UVIKO-19 endapo mtu ataambukizwa”. Amesema Prof. Makubi.
Aidha, Prof Makubi amesema mwitikio wa wananchi kujitokeza kupata chanjo baada ya kuanzishwa kampeni hiyo ni mkubwa ambapo baada ya kuzinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan idadi ya waliochanjwa ilikua ni 28,000 nchi nzima lakini baada ya kampeni Mpya ya jamii shirikishi watu zaidi ya 850,000 wamechanjwa mpaka jana, huku akielezea sasa kuwa kwa sasa watu takiribani 50, 0000 wanachanjwa kila siku
Prof. Makubi amesema Kampeni ya jamii harakishi na shirikishi ilizinduliwa kwa lengo la kuhamasisha jamii kuchanja katika maeneo mbalimbali ikiwemo makanisa, misikiti, makundi mengine kama wanamichezo, makazini, masokoni, kwenye kaya na sehemu zote zenye mikusanyiko kuanzia mijini mpaka vijijini