………………………………………………..
Na.WAMJW-IRINGA
Ili kufikia hatua kubwa ya kinga kundi na kuweza kuwasaidia wanachi kuwakinga na maambukizi ya UVIKO-19, Tanzania tunapaswa kufikia asilimia 60 ya watanzania wawe wamepata chanjo dhidi ya UVIKO-19.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Queen Sendiga wakati wa kikao cha kamati ya afya ya msingi cha uraghibishaji wa mpango jumuishi, harakishi wa utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwenye ukumbi wa Siasa ni kilimo uliopo mkoani hapa.
Mhe. Sendiga amesema kuwa watanzania wakiwa wamechanga kwa asilimia hiyo itasaidia kupunguza maambukizi pamoja na vifo vingi na kutolea mfano kwa mkoa wa Iringa ni miongoni walioathirika katika wimbi hili la tatu na kwamba wamepata vifo kutokana na ugonjwa huo.
“Tumepata vifo vingi,tumepoteza ndugu na jamaa zetu kutokana na ugonjwa huu na vile vile tumepoteza hadi vijana hivyo tumeona hali ilivyokua ngumu, kwahiyo kutokana na mpango huu wa Wizara na TAMISEMI tunapaswa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wetu na kuwafikia wananchi wengi ili kuwaokoa wanachi wetu na janga hili”Alisisitiza .
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa huyo aliwathibitisha wajumbe wa kikao hicho kwamba yeye pamoja na wataalam wake wameshapata chanjo hiyo na hadi sasa wanaendelea vizuri licha ya upotoshaji unaosambazwa na baadhi ya watu na mitandao ya kijamii”Naomba niwahakikishie chanjo hii ni salalama na haina madhara yeyote kwani imethibitishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Ameongeza kuwa mkoa wake umejipanga kutoa elimu na kuwafikia wananchi wote kila mahali na kuwataka washiriki hao kuwa mabalozi wazuri wanaporudi majumbani ili kuwaokoa wanachi wanaowazunguka.
Mhe. Sendiga amesema kuwa katika kutekeleza mpango huo hivi sasa mkoa wake umeongeza vituo vya kutolea chanjo ya UVIKO-19 kutoka vituo 25 hadi kufikia vituo 231 na wataalam wameanza kutoa elimu kwa wanachi na kutoa huduma ya chanjo hiyo kila mahali.
Naye,Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Happiness Seneda amesema kuwa tangu kuanza kwa zoezi la uhamasishaji na uelimishaji wa ugonjwa huo na chanjo mkoani hapa idadi ya wananchi waliochanjwa imeongezeka na kwa kiasi kikubwa uelewa umeanza kuongezeka kwa jamii.