Mbunge wa jimbo la Igunga ,Nicholaus Ngassa akizungumza na wananchi wa Mwamashiga wilayani Igunga mkoani Tabora.
…………………………………
Na Lucas Raphael,Tabora
Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini,Tarura,Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Sadick Karume amesema kwamba wanakusudia kutumia Kiasi Cha Sh350 milioni kutengeneza daraja la mto Mwamashiga,lililopo wilayani Igunga ambalo limebomoka zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Igunga ,Nicholaus Ngassa,alisema fedha hizo zitatosha kujengwa daraja hilo kuanzia mwezi Novemba mwaka huu.
“Katika fedha shilingi bilioni moja na nusu,tutatengeneza daraja hilo na mengine mawili pamoja na barabara zinazounganisha kata”Amesema
Mbunge wa Igunga,Nicholaus Ngassa,alisema daraja hilo limekuwa likikata Mawasiliano ya kata Tano kipindi Cha masika na kuwaathiri wananchi kiuchumi,kiafya na kijamii.
Alishukuru utaratibu wa wabunge kuchagua barabara na madaraja ya kutengenezwa,Akisema wamelipa kipaumbele daraja hilo pamoja na barabara zinazounganisha kata.
“Tunataka wananchi wanaoathirika na kukatika daraja hilo hasa kipindi Cha masika ambacho ndio kinakaribia,waondokane na adha hiyo”Amesema
Wakazi wa kata ya Mwamashiga,walidai kuwa wanateseka kipindi cha masika kwa kutengwa na maeneo mengine na kujengwa daraja hilo kutakuwa mkombozi kwao.
“Huwa tunapata shida kubwa ya kufuata mahitaji au kupeleka bidhaa zetu maeneo mengine kutokana na kukatika daraja hilo”Amesema Mwanaidi Shaban mkazi wa kata ya Mwamashiga
Zaidi ya watu elfu sabini wa kata Tano wanaathirika kwa kukatika daraja hilo,kiafya,kielimu na kiuchumi na kujengwa kwake kutawakomboa.
Mbunge Ngassa yupo katika ziara ya kutembelea vijiji kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.