Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
………………………………
Msimamizi Mkuu wa Mchaguzi jimbo la Shinyanga Mjini Jomary Satura ametoa wito kwa wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua kiongozi bora mwenye sifa ya kuwaletea maendeleo
Amesema wananchi wahamasike kwa kutumia haki yao yakikatiba kumchagua kiongozi ambaye wanaamini atawasaidia katika jitihada za kuchochea maendeleo
Satura amesema tayari maandalizi ya mchakato huo wa uchaguzi yameanza yakitanguliwa na vikao vinavyohusisha viongozi wa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kwa lengo la kukumbushana kanuni na taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa
“Tumetoa mialiko kwa vyama vyote vya siasa vilivyopo ndani ya jimbo letu la Shinyanga ili wahudhulie kikao cha leo cha maandalizi ambacho kimefanyika kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana,
Kanuni za maadili ya uchaguzi vinatutaka tukae na vyama vya siasa tukumbushane mambo ya msingi ya kuzingatia lengo tukumbushane taratibu, sheria na kanuni za uchaguzi ambayo pia ni masuala ya kimahusiano kuweka urafiki pamoja lakini tunakumbushana kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi kwa sababu sisi ni watanzania ni muhimu tufanye uchaguzi wenye amani, uhuru kwa kuheshimiana” amesema Satura
Satura ameeleza kuwa kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi huo mdogo wa nafasi ya udiwani kata ya Ndembezi wilaya ya Shinyanga Mjini, Septemba 13 hadi 19 ni uchukuaji wa fomu ambapo uteuzi wa wagombea utafanyika Septemba 19 na kwamba uchaguzi utakuwa Oktoba 09, Mwaka huu 2021
Mchakato huo unafuatia aliyekuwa Diwani wa kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga David Nkulila kufariki Dunia hivi karibuni ambaye pia alikuwa ni meya wa Manispaa ya Shinyanga