Baadhi ya waandishi wa habari na watendaji wa chama cha TANFLEA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa NIMR jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Maalum
Waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari zaidi ya 20 nchini, wamepewa mafunzo ya kuwajengea uelewa kuhusu Epidemiolojia, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Epidemiolojia Duniani.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanya Septemba 7, 2021 kwa mara ya kwanza duniani kote ambapo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Jijini Dodoma huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.
Yameelezwa hayo leo na Rais wa Chama cha Wataalamu wa Udhibiti na Ufuatiliaji wa Magonjwa Tanzania (TANFLEA), Elibariki Mwakapeje alipozungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Dar es Salaam.
Amesema wanahabari ni kundi muhimu la kushirikiana nalo kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi hususan jinsi ya kujikinga na magonjwa mbalimbali.
“Wameitikia kwa wingi, mafunzo haya yalihusu zaidi kuwajengea uwelewa kuhusu Epidemiolojia na Maadhimisho ya Siku ya Epidemiolojia Duniani ambayo yatafanyika kwa mara ya kwanza duniani kote ,” amesema.
Dk. Mwakapeje amesema siku hiyo itaambatana na shughuli mbalimbali ikiwamo uchunguzi wa afya (afya check) kwa wananchi bila malipo pamoja na uchangiaji damu, viwanja vya Nyerere Square.
“Tunahimiza wananchi wajitokeze kwa wingi siku hiyo ili waweze kupima afya zao, tutapima shinikizo la damu {la juu na la chini}, uwiano wa urefu na uzito na huduma nyinginezo, tunawakaribisha wote,” ametoa rai.
Ameongeza “Ndiyo maana leo tumewaita wanahabari kuwajengea uwelewa kuhusu Epidemiolojia hususan maadhimisho ya siku hii, tunashukuru kwamba semina yetu imeenda vizuri.
“Tumepata mafanikio kwa sababu imetuongezea wigo wa kufanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari ili tuweze kukitangaza chama hiki na tuweze kufanya kazi nao nchini mzima kuhamasisha jamii masuala ya afya na iweze kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwamo UVIKO – 19, janga ambalo sasa linaisumbua dunia.
“Lengo pia ni tuzidi kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa matukio ya kiafya katika jamii ili tuweze kutambua na kukabiliana na matukio hayo kwa haraka zaidi.
“Aidha, kuendelea kuweka msisitizo ili afya za watanzania zizidi kuimarika, hatimaye washiriki shughuli za uzalishaji mali ili kuweza kuinua uchumi katika ngazi za familia na jamii kwa ujumla,” amebainisha.
Amesema Chama hicho kilianzishwa na kusajiriwa Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, mnamo mwaka 2014, na kupata namba ya usajiri No. S. A. 19455.
Amesema hadi kufikia sasa, Septemba 2021, kina jumla wa wanachama 152 –ambao ni wahitimu wa Shahada ya Uzamili wa Applied Epidemiology and Laboratory Management kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Amesema wanachama hao pia ni watumishi wa Umma, Mashirika ya Kimataifa na yale yasiyo ya Kiserikali ambao wapo Tanzania bara na Zanzibar, pia chama hiki kinafanya kazi chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Naye, Dk. Ali Hussein kutoka TANFLEA na Mwanakamati wa machapisho ya chama hicho, amefafanua kwamba Epidemiolojia ni fani ya sayansi ambayo inahusika na kutambua magonjwa, visababishi vya magonjwa na jinsi magonjwa yanavyosambaa katika jamii.
Amesema tangu 2014, kufikia sasa ni miaka saba na kwamba kimekuwa kikitoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu wa Epidemiolojia nchini.
“Kila mwanafunzi lazima afanye tafiti na hadi sasa wameshafanya zaidi ya tafiti 100, kutokana na mafunzo waliyosoma katika program maalum,” amesema Dk. Hussein ambaye pia ni miongoni mwa walimu katika kozi hiyo.
Ameongeza “Wanafanya uchunguzi wa magonjwa yanayotokea ya mlipuko pamoja na kuchakata takwimu zinazokusanywa katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya.
“Kwa mfano magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Malaria, magonjwa ya kuambukiza na hata yasiyoambukiza,” amebainisha.
Akizungumza, Silvano Kayela kutoka Mlimani Media (Tv na Redio) ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo amesema “Ni mazuri, wametueleza wamekuwepo 2014 na kumekuwa na ukimya sana, sisi wenyewe wana habari hatukuwa na uelewa na kitu ambacho wanakifanya.
“Hivyo yametufumbua hata sisi kujua nini wanachokifanya na itaturahisishia sisi kukipeleka kwa jamii kwa sababu sisi ni muunganiko kati ya jamii na wataalamu au jamii na mamlaka kwa hiyo nafkiri hii itakuwa fursa nzuri ya kufungua njia ya uelewa kwa jamii.
Maadhimisho ya kwanza ya Epidemiolojia Duniani yamepewa kauli mbiu isemayo “Kuimarisha Mifumo ya Ufuatiliaji wa Magonjwa na Matukio Yanayoathiri Afya ili Kutambua Mapema Viashiria Hatari vya Afya kwa Jamii, (Strengthen Health Surveillance System for Early Detection of Public Health Threats)”.