Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akikata utepe kuzindua kituo cha redio cha Gold FM mjini Kahama Mkoani Shinyanga pembeni yake ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa Katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki hafla ya uzinduzi wa kituo cha redio cha Gold FM mjini Kahama Mkoani Shinyanga pembeni yake kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga, wa kwanza kushoto ni Bi Neema Mghen, Mkurugenzi wa kituo cha Gold FM na wa mwisho kushoto ni Mhnadisi Francis Mihayo Mkuu wa TCRA kanda ya ziwa.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akiwa katika studio za kituo cha redio cha Gold FM mjini Kahama Mkoani Shinyanga.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza katika mahojiano maalum na Juma Diwani mtangazji wa kipindi cha asubuhi maarufu kama Gold breakfast mara baada ya uzinduzi rasmi wa kituo hicho.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa akizungumza na watangazaji na wageni walioshiriki hafla ya uzinduzi wa kituo cha redio cha Gold FM mjini Kahama Mkoani Shinyanga.
……………………………………………………………………….
Na: Projestus Binamungu,WHUSN KAHAMA
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uhuru wa vyombo vya habari akisisitiza uhuru huo kuenda sambamba na wajibu.
Waziri Bashungwa ametoa kauli hiyo Septemba 3 2021, wakati akizindua kituo cha matangazo mjini Kahama mkoani Shinyanga kilichopewa jina la Gold Fm ikiwa na kauli mbiu ya Sauti ya dhahabu.
Akizungumza katika mahojiano maalum mara baada ya uzinduzi wa kituo hicho Waziri Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Rais Samia Suluhu Hasaan inathamini na kuamini katika uhuru wa vyombo vya habari kupaza sauti za watanzania ili kuyafikia matamanio yao.
Waziri Bashungwa amesema “Serikali ya awamu ya sita kwa kuthamini uhuru wa vyombo vya habari inakusudia kuondoa asilimia 50 ya ada za tozo mbalimbali za leseni kwenye marekebisho ya kanuni za maudhui ya mtandaoni na maudhui ya utangazaji katika redio na televisheni”
Ameongeza kuwa “Wamiliki wa mitandao ya kijamii kama YouTube ambayo maudhui yake siyo ya kihabari wataruhusiwa kupakia video zao mitandaoni bure, kama sehemu ya kuwawezesha kujitangaza na kujiingizia kipato zaidi”.
Akizungumzia uwekezaji huo waziri Bashungwa amekaliliwa akisema “Ninafurahi kuona uwekezaji wa namna hii unaenda sehemu husika (Kahama), na endapo mtahitaji kuanzisha television nawashauri mkiweza anzeni mapema na mkihitaji msaada tuambieni hiyo ndiyo kazi yetu”
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amezungumzia maendeleo ya mchakato wa kupata vazi la taifa amesema Serikali kupitia wizara yake inakusudia kuwakutanisha wabunifu wa mavazi wa hapa nchini na kuwapa fursa ya kubuni vazi litakalo shindanishwa na kupigiwa kura ili kupata mavazi kadhaa yatakayotumika kama mavazi rasimi ya kumtambulisha mtanzania.
“Serikali iliona ni vyema iandae utaratibu ambao kupitia kwa wabunifu wa mavazi wenye wabuni na waseme kuwa hili linafaa kuwa vazi la taifa, na vazi hili siyo lazima liwe moja, yanaweza kuwa hata mawili n ahata matatu lakini yale ambayo yatashindanishwa na kushinda” alisema Waziri Bashungwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo amewataka watangazaji na waandishi wa habari kuwa wabunifu zaidi ili kuitendea haki leseni ya utangazaji inayotolewa na mamlka hiyo kwa nia ya kuwawezesha watanzania kuhabarishwa kwa ubunifu zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Gold FM Bi Neema Mghen ameiomba Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Sanaa Tanzania BASATA kwa kushirikiana na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA kuvijengea mazingira wezeshi vituo vichanga vya redio ili viendelee kuwa daraja la kuwasaidia wasanii wachanga kutimiza ndoto zao.
Uzinduzi wa kituo hicho cha redio cha Gold FM kinaifanya wilaya ya Kahama kuwa na vituo Vinne vya redio huku kwa mkoa wa Shinyanga vikifika vituo vitano ambavyo ni redio Gold FM, Kahama FM, Divine FM, Huheso FM na Radio Faraja Fm.