Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akibeba zege akishiriki katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Msisima iliyopo Wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikabidhi mifuko ya saruji katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Msisima iliyopo Wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na wananchi wa Kata ya Msisima Wilayani Namtumbo wakati wa ziara yake mkoani Ruvuma.
Picha zote na Kitego cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
*************************
Na Mwandishi Wetu Namtumbo
Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameungana na wananchi wa Kata ya Msisima kushiriki ujenzi wa Shule ya Sekondari katika Kata hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuamsha Ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Namtumbo ameitaka jamii kuendelea kuongezea nguvu katika kushiriki katika shughuli za maendeleo kwani ndio itasaidia kutatua changamoto mbalimbali.
Naibu Waziri Mwanaidi amewataka viongozi wa Wilaya ya Namtumbo kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za wananchi katika kukamilisha miradi mbalimbali ili iweze kuhudumia wananchi kama upatikanaji wa huduma za Afya, Elimu na maji.
“Nimejionea mwenyewe umbali kufika hapa huduma hii ya Shule inahitajika sana maana Watoto wetu wanaifuata mbali sana kutoka katika Kata hii, Wilaya naomba muunge mkono jitihada hizi wananchi wapate maendeleo” alisema Mhe. Mwanaidi
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Msisima wameseama kuwa wamehamasika katika kujitolea katika shughuli za maendeleo kwani waliona changamoto za umbali wa watoto kwenda shule na kuamua kuanzia ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mhe. Dkt. Julius Kenneth Ningu amesema Wilaya itaendelea kuhamasisha wananchi wa Wilaya hiyo kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuongeza nguvu pale watakapokwama.
Ameongeza kuwa Wilaya itaendelea kusimamia na kuhakikisha vitendo vya ukatili vinadhibitiwa hasa mimba za utotoni na kuhakikisha wahanga wanapata huduma stahiki na Sheria inachukua mkondo wake na haki inapatikana.
Aidha Naibu Waziri Mwanaidi amezungumza na watendaji wa Dawati la Polisi la Wanawake na Watoto pamoja na watendaji wengine wanaosimamia masuala ya ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto Wilaya ya Namtumbo na kuwataka watendaji hao kusimamia Sheria katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa mimba za utotoni kwani ni suala la hatari kwa Ustawi wa Watoto hao.
“Nimepata taarifa Watoto 177 wamepata mimba hakikisheni hawa wote waliohusikia wanapatikana na kuchukuliwa hatua maana wameharibu ndoto za watoto wetu hawa” alisema Mhe. Mwanaidi
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi amevitembelea vikundi vya Wajasirimali Wanawake katika Wilaya ya Namtumbo na kuitaka Wilaya hiyo kuendelea kuongezea nguvu katika kuwawezesha kupata mikopo inayotolewa na Halmashauri na kuwasaidia kupata masoko ya bidhaa zao.