Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akishiriki kuchanganya zege katika zoezi la ujenzi wa jengo la Maabara ya Shule ya Sekondari Mdeme iliyopo Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akishiriki ujenzi wa katika zoezi la ujenzi wa jengo la Maabara ya Shule ya Sekondari Mdeme iliyopo Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
******************************
Na Mwandishi Wetu Mbinga
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wazazi wanaowakosesha Watoto haki ya msingi ya kuendelezwa kwa kupata elimu.
Ameyasema hayo Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakati akishiriki zoezi la ujenzi wa jengo la Maabara katika Shule ya Sekondari Mdeme.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali imechukua jukumu la kulipia gharama za Shule kuanzia Shule ya Msingi mpaka kidato cha nne hivyo hawana sababu ya kutowapeleka Watoto Shule kupata elimu.
Ameongeza kuwa Watoto ndio taifa linalotegemewa kuongoza Taifa kwa vizazi vijavyo hivyo Jamii ina wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata elimu na kukingea na vitendo vya kikatili hasa kuepukana na mimba za utotoni.
“Vitendo vya ukatili kwa Watoto wetu vimekithiri hasa mimba za utotoni ambazo zinasababisha Watoto kutoendelea na shule na kukatisha ndoto zao Jamii pambaneni na vitendo hivi tuwaokoe Watoto wetu” alisema Naibu Waziri Mwanaidi.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Jengo la Maabara ya Shule ya Sekondari Mdeme Mtendaji wa Kata ya Amani Makoro Joachim Kaponda amesema wananchi wamehamasika sana kujitolea katika shughuli za Maendeleo kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo amemuhakikishia Naibu Waziri kusimamia miundombinu mbalimbali inayojengwa kwa nguvu za wananchi na kuhakikisha watoto wanapata elimu na wazazi wanawajibika kuwapeleka Watoto wao shule.
Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi ameshiriki katika Kampeni ya Piga Kazi Boresha Makazi katika Kijiji cha Mapera Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma na kuwahamasisha wananchi kuboresha Makazi yao kuondokana na madhara na magonjwa yanayotokana na kuwa na Makazi duni.
Katika ziara yake Wilayani Mbinga Naibu Waziri Mwanaidi pia amekitembelea Kikundi cha Wanawake Wajasirimali cha Amani VICCOBA Lukarasi na kujionea shughuli za ukamuaji wa mafuta ya Alizeti.