Na Happiness Shayo –Madaba- Songea
Wananchi wa Halmashauri ya Mabada Mkoani Ruvuma hususan katika vijiji vya Wino, Igawisenga, Lilondo, Mkongotema, Lutikila, Magingo, Maweso na Ifinga wataendelea kunufaika kiuchumi kutokana na uzalishaji wa miti katika Shamba la Miti Wino linalomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika mkutano na wananchi wa vijiji vinavyolizunguka shamba hilo uliofanyika katika ofisi ya TFS, Madaba-Songea.
“Serikali kwa kutambua mchango wenu katika kusaidia uhifadhi wa shamba hili, hatutasita kuwaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na ujenzi wa mabweni kwenye shule za sekondari ”amesema Mhe. Masanja.
Ameongeza kuwa kupitia shamba hilo wanavijiji hao watanufaika na ajira za muda mfupi na mrefu zinazotokana na kuisaidia TFS kupanda miti, kusafisha shamba kwa kufyeka na kufanya palizi ya shamba la miti Wino.
Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa Serikali itaboresha miundombinu ya maeneo yenye umuhimu sana ya vijiji hivyo katika mwaka huu wa fedha kwa kushirikiana wananchi hao ili maendeleo ya Madaba yasonge mbele.
Aidha, Mhe. Masanja ameahidi kutatua changamoto ya kitalu cha uwindaji cha Wembele ambacho kimesitisha kutoa gawio kwa vijiji vilivyo katika eneo hilo na kuahidi kuhakikisha fedha za uwindaji wa kitalii zinazopatikana ziwanufaishe wananchi hao.
Kuhusu changamoto ya moto wa msituni unaotokea katika shamba hilo, Mhe. Masanja ameelekeza watendaji wa vijiji, kata na madiwani wa eneo hilo kuelimisha wananchi wao kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa uongozi wa shamba wanapotaka kusafisha mashamba yao ili kuepuka moto pori.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Wino, Hezron Mwageni ametoa ushuhuda wa kuwepo kwa shamba la miti Wino kwamba limesaidia kujenga mradi wa maji katika kijiji cha Ifingo.
Pia, memshukuru Msimamizi wa shamba hilo kwa kuendelea kutoa miche ya miti bure kwa wanavijiji wa eneo hilo.
“Shamba hili la miti Wino kupitia TFS limekuwa likitupatia miche ya miti kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba yetu katika vijiji vya Wino, Igawisenga, Lilondo, Mkongotema na hili ni jambo la heri sana kwa sababu hii linawafanya wananchi wawe walinzi katika mashamba ya miti”ameongeza Bw. Mwageni.
Ameelezea kuwa TFS imekuwa msaada mkubwa kwa kusaidia katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya wanavijiji hao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makanisa , shule za sekondari na shule za msingi.
Awali akiwasilisha taarifa ya shamba hilo, Mhifadhi wa Shamba la Miti Wino, Lucas Manyonyi amesema shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 39,000 limefanikiwa kujenga mradi wa maji mtiririko uliogharimu shilingi milioni 482 katika kijiji cha Mkongotema.
Amesema mafanikio mengine yaliyopatikana ni kutoa ajira za muda mrefu na mfupi kwa wanavijiji takribani 4000 kila mwaka katika shamba la miti Wino.
Bw. Manyoni amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kutokana na uzalishaji wa miti katika shamba hilo viwanda vingi vya kuchakata mazao ya misitu vitasimikwa katika maeneo ya Halmashauri ya Madaba.
Mkutano huo wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja umehudhuriwa na wananchi wa Halmashauri ya Madaba, Watendaji wa Vijiji, Madiwani ,Watendaji na baadhi ya watumishi wa TFS.