Kutawaliwa kifikra kwa waafrika kwa ujumla kumeelezwa yakuwa ndio chanzo kikubwa cha kudorola kwa maendeleo katika nchi zilizopo kwenye bara hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mtaalamu wa Sheria nchini Kenya Profesa Patrick Lumumba, wakati wa kufunga Tamasha la 11 la kitaaluma la kigoda cha Mwalimu Nyerere iliyofanyika katika ukumbi wa Nkurumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Lumumba, amesema kuwa licha ya utajiri wa rasilimali uliopo Afrika lakini bado bara hilo limeghubukwa na kutawaliwa kifikra hali inayosababisha hali duni kiuchumi katika baadhi ya nchi zilizopo katika bara hilo.
“Bado Waafrika tumetawaliwa hata kama tunajiona tuko huru lakini utawala mbovu wa fikra unatusumbua kiasi cha kushindwa kutumia tulivyonavyo kujiinua na hatimaye tunajivunia vigeni”. Amesema Prof. Lumumba.
Pamoja na hayo Profesa Lumumba ameongeza kuwa ili kukabiliana na hilo ni wajibu kuunda mifumo mipya ya elimu itakayoasisiwa na Waafrika wenyewe kwani ndiyo wanaojua uhalisia wa Mataifa yake.
“Huwa nashangazwa sana ninaposafiri kutoka Kenya kwenda taifa lolote la Afrika natakiwa kujaza nyaraka nyingi pia nikifika bado nakabiliwa na kubadilisha fedha kuwa ya taifa hilo vilevile mtandao wa simu kwa ajili ya mawasiliano hivi sivyo waasisi wetu walihitaji”. Amesema Prof. Lumumba.
Aidha, Prof. Lumumba amesema kuwa waasisi walikuwa na lengo la kuleta umoja wa Afrika lakini kwa sasa umevurugwa kutokana na kuwepo kwa matabaka ambayo yamesababisha kila taifa kujitegemea na vilevile hakuna haja ya kila taifa la Afrika kuwa na fedha binafsi kulipaswa kuwe na fedha moja ambayo ingetumika Afrika nzima.
Vilevile Prof.Lumumba ameongeza kuwa ukombozi wa Afrika uhusishe kufundishwa maisha halisi ya Afrika ili kumtengeneza kiongozi mwenye uzalendo na Afrika badala ya kusoma kwenye vitabu ambavyo vimetungwa na wasio wa Afrika.
“Kiongozi anajengwa tangu akiwa mdogo hivyo ni vyema tukabadili mifumo yetu ya ufundishaji ambayo ilikuwa inamlemaza mtoto kusoma vitabu badala ya kupata uhalisisa wa Bara letu”. Ameongeza Prof.Lumumba.