Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa (Mb) amemuomba Balozi wa Tanzania nchini Kuwait Mhe. Mhandisi Aisha S. Amour kuendeleza Uhusiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Kuwait, kwa kuona jinsi gani pia Taifa hilo linaweza kusaidia kuboresha miundombinu katika Shule mbalimbali za Michezo nchini.
Mhe.Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 13 Julai, 2021 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Aisha katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo pia amemuhakikishia Mheshimiwa Balozi kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana naye bega kwa bega katika masuala yote ya kimichezo yatakayoendeleza ushirikiano mwema baina ya nchi hizo mbili.
“Mheshimiwa Balozi kwanza tu nikuhakikishie kuwa Wizara ipo tayari kushirikiana nawe katika masuala yote ya kimichezo ambayo yataendeleza ushirikiano mwema baina ya Tanzania na Kuwait, lakini pia tuomba utusaidie kuona ni kwa jinsi gani Taifa hilo litatusaidia kuboresha miundombinu katika shule zetu za michezo nchini, ili kuendelea kuibua vipaji zaidi mashuleni na hususani katika mashindano ya Umisseta na Umitashumta,”amesema Mhe. Bashungwa.
Kwa upande wake Mhe. Aisha Amour amesema Serikali ya Kuwait ipo tayari kuendeleza Uhusiano mzuri uliopo kwa kushirikiana na Tanzania katika michezo pamoja na Sanaa, huku akisisitiza kufanyika kwa mchezo wa Kirafiki wa mpira wa miguu baina ya timu za mataifa hayo, jambo ambalo litatangaza Utalii na kupelekea ajira ya wachezaji nje ya nchi.
“Mheshimiwa waziri nikuombe ulisimamie hili la kuandaa mchezo wa kirafiki baina ya mataifa haya mawili, kwa sababu wenzetu wapo tayari, na hii itatusaidia pia kukuza uchumi wetu kwa kuingiza fedha za kigeni pamoja na kutangaza Utalii tulionao nchini, na labda pia wachezaji wetu wanaweza kupata soko nje ya nchi kwa kupitia ushirikiano huu,”amesema Mhe. Aisha.