Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba na Wabunge wa Muleba baada ya kumaliza ziara yake ya siku nne mkoani Kagera kwa lengo la kutatua migogoro iliyokuwepo kwenye maeneo yanayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenarali Charles Mbuge na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Meja Jenarali Charles Mbuge (wa tatu kutoka kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kutoka kulia), Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila (wa pili kutoka kushoto), Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Mhe. Dkt. Oscar Kikoyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Muleba, Bw. Emmanuel Sherembi wakiwa wameshikilia nakala za maazimio yaliyoafikiwa kuhusu utatuzi wa mgogoro wa ardhi kwenye Mradi wa Mwisa II uliopo wilayani Muleba.
………………………………………………………….
Ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki mkoani Kagera imekuwa dawa ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Waziri Ndaki amefanya ziara ya siku nne mkoani Kagera kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi iliyokuwepo katika maeneo yanayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Ranchi za Mabale wilayani Misenyi, Kagoma na Mwesa wilayani Muleba mkoani Kagera.
Akizungumza na uongozi wa mkoa wa Kagera ambapo pia alikuwepo Katibu Mkuu anayesimamia sekta ya mifugo baada ya kumaliza ziara yake, Waziri Ndaki alisema kuwa ziara hiyo imekuwa muhimu na yenye mafanikio makubwa kwake na kwa sekta ya mifugo kwani uwepo wa migogoro husababisha kupungua kwa kasi ya ukuaji wa sekta ya mifugo.
Katika ranchi hizo kulikuwa na wananchi ambao walikuwa wanakaa kwa muda mrefu na kufanya shughuli zao za maendeleo katika maeneo hayo. Hivyo kutokana na hilo kulikuwepo na migogoro kati ya wananchi hao na wawekezaji waliopewa vitalu kwa ajili kufugia mifugo.
Baada ya malalamiko hayo ya muda mrefu kati ya wananchi na wawekezaji, Waziri Ndaki aliwaeleza wananchi hao kuwa Mhe. Rais Samia Hassan ameridhia wabaki katika maeneo hayo na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo. Pia aliwaeleza wananchi na wawekezaji kuwa serikali itayapima upya maeneo hayo na kuweka alama za mipaka ili migogoro hii isijirudie.
Vilevile wananchi katika maeneo hayo walielezwa kuwa upimaji na mipaka ikishawekwa lazima kila mmoja aifuate na kuiheshimu. Pia kwa wale ambao wamejitenga mmoja mmoja wanatakiwa kuanza kuhama na kutafuta maeneo kwenye vijiji.
Waziri Ndaki pia aliwaeleza wawekezaji kuwa upimaji huu utakaofanyika katika maeneo ya ranchi hauta waathiri katika shughuli zao za ufugaji. Serikali inawahitaji wawekezaji katika kuhakikisha sekta ya Mifugo inakua. Lakini pia amewasisitiza wawekezaji kuwa vitalu watakavyopewa ni lazima wahakikishe wanavitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuhakikisha wanafuga mifugo bora.
Katika ranchi ya Mwisa II ambayo nayo ilikuwa na mgogoro mkubwa Waziri Ndaki alisema tayari wizara imeshaweka makubaliano na uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Wilaya ya Muleba ili kuhakikisha utatuzi wa mgogoro uliopo pale unatatuliwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenarali Charles Mbuge amesema kuwa ulinzi na usalama ni kipaumbele namba moja kwenye mkoa hivyo uwepo wa migogoro husababisha uvunjifu wa amani. Hivyo utatuzi wa migogoro uliofanyika utasaidia sana maeneo hayo kuwa na amani na kuwafanya wananchi na wawekezaji kuendeleza shughuli zao za maendeleo. Kwa upande wake ameahidi kuwa atasimamia utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa katika utatuzi wa migogoro hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage na Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Oscar Kikoyo walisema kuwa migogoro hiyo imechukua muda mrefu kutatuliwa lakini wamemshukuru Mhe. Rais Samia Hassan kwa kuridhia wananchi hao kubaki katika maeneo hayo yanayomilikiwa NARCO. Vilevile wamemshukuru Waziri Ndaki na viongozi na wataalam katika Wizara Mifugo kwa jitihada waliochukua ili kuhakikisha wanamaliza migogoro hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha sekta ya mifugo inakua na inaongeza kipato kwa wafugaji na taifa kwa ujumla. Pia alisema kwa upande wa wizara atahakikisha makubaliano yote yaliyofikiwa yanakwenda kutekelezwa.
Utatuzi wa wa migogoro hiyo katika Mkoa wa Kagera umeleta faraja kubwa kwa wananchi ambao walikuwa wanakaa katika maeneo ya ranchi za Taifa. Lakini pia kwa wawekezaji waliopatiwa vitalu kwani baada ya utatuzi huo sasa pande zote mbili watafanya shughuli zao za kiuchumi kwa amani.