Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwasili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ringa na kupokelewa na Viongozi waandamizi ya Hospitali hiyo kwa ziara ya kikazi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Sr. Dkt. Scolastica Malangalila akimtambulisha Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwa Viongozi Waandamizi wa Hospitali hiyo mara baada ya kuwasili Hospitalini hapo kwa Ziara ya kikazi.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Sr. Dkt. Scolastica Malangalila akiwasilisha Taarifa ya hospitali mbele ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea Hospitali hiyo.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
*************************
Na Mwandishi wetu, Iringa
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi watatu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa wanaodaiwa kushirikiana na mawakala wa Benki kuchepusha kiasi cha takribani milioni ishirini kwa ajili ya ununuzi wa dawa Hospitalini hapo.
Ametoa agizo hilo katika kikao na Watendaji waandamizi wa Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake Mkoani Iringa ambapo alipata taarifa kutoka vyanzo maalum kuwa baadhi ya watumishi wanashirikiana na mawakala wa Benki kuchepusha fedha za Hospitali kwenda kwenye akaunti zao binafsi.
“Nimesikia taarifa ya hospitali lakini nahoji, sikusikia taarifa za upotevu wa fedha za Hospitali kupitia akaunti za watumishi wa hapa au sio Hospitali hii?” alihoji Niabu Waziri Mwanaidi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa katika hospitali hivyo yeye kama msaidizi wa Rais katika Sekta husika hatofumbia macho vitendo vyovyote vya ubadhirifu wa fedha za umma.
Aidha Naibu Waziri Mmwanaidi ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilkifu matumizi ya fedha zinazoletwa na Serikali kwa malengo ya kutoa huduma kwa wananchi na sio kujifunaisha watu wachache.
“Niseme hatuwezi kuvumilia haya madudu kabisa fedha zinatolewa na Serikali kuja kutoa huduma kwa wananchi wewe mtumishi wa Umma unajimilikisha hili hapana tunashughulika nalo” alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Abbas Idd amesema ni kweli tukio hilo limetokea na linafanyiwa kazi na vyombo vya uchunguzi ili kubaini wale wote waliohusika na kuweza kuwachukulia hatua.
“Mheshimiwa Naibu Waziri kulikuwa na matukio mawili tofauti lakini kama ni suala hilo, kweli kuna baadhi ya wafanyakazi wenzetu wamebainika kushirikiana na baadhi ya mawakala wa Benki na kuhamisha fedha za malipo ya dawa kwenda kwenye akaunti zao binafsi,” alisema Abbas.
Baada ya maelezo hayo, Naibu Waziri Mwanaidi akaagiza kudhibitiwa kwa Akaunti za watumishi na mawakala wa Benki waliohusika na kuhakikisha kwamba uchunguzi wa kina unafanyika ili kuepusha udanganyifu wa aina hiyo kuendelea kutokea na Mawakala wa Benki walioshirikiana na watumishi wa Hospitali hiyo kuchepusha fedha za umma kulipa fedha hizo ili kufidia hasara iliyopatikana.
Awali akiwasilisha taarifa ya Hospitali, Kaimu Mganga Mfawidhi Sr. Dkt. Scolastica Malangalila alisema Hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa huduma za kibingwa kutokana na kutokuwa na madaktari wa fani hizo.
Akiwa Hospitalini hapo, Naibu Waziri huyo alitembelea Kitengo maalum kwa ajili ya huduma kwa Wazee, Huduma ya Mama wajawazito na Wazazi pamoja na Watoto wanaopata huduma za uangalizi maalum kutokana na matatizo mbalimbali.