Ni jengo la TANESCO Mkoa wa Ruvuma.
Baadhi ya watumishi wa TANESCO wakiongozwa na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Florence Mwakasege walipotembelea ofisi ndogo ya TANESCO Madaba wilayani Songea
kituo cha kupozea umeme wa gridi kilichopo Unangwa mjini Songea
…………………………………………………………………..
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) limefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji 119 kati ya lengo la kusambaza umeme vijiji 161.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Florence Mwakasege amesema mradi huo umetekelezwa kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza ukihusisha pia ujenzi wa njia mbili za umeme wenye urefu wa Kilometa 106 kuelekea kituo cha kufua umeme wa maji Nakatuta Mto Ruvuma.
Amezitaja gharama za mradi huo kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 43 na kwamba vijiji ambavyo bado havijasambaziwa umeme utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali.
Mhandisi Mwakasege amesema tayari wateja 5,902 wa awali wameunganishiwa kati ya lengo la kuunganishiwa wateja 6,178 mradi huo utakapokamilika kwa asilimia 100
Amesema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vijiji 551,kati ya hivyo vijiji vyenye umeme ni 295,vijiji visivyo na umeme vilivyoomba kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa pili 256 na vijiji vitakavyokuwa na umeme baada ya miradi inayoendelea kukamilika ni 295.
Hata hivyo amesisitiza kuwa hadi kufikia Desemba 2022 vijiji vyote ambavyo havijapatiwa umeme katika Mkoa wa Ruvuma vinatarajiwa kumfikiwa na umeme.
Kuhusu upatikanaji wa umeme mkoani Ruvuma,Mhandisi Mwakasege amesema upatikanaji wa umeme ni wa kuridhisha baada ya Mkoa kuunganishwa na Grid ya Taifa katika Wilaya za Songea,Namtumbo,Mbinga,Nyasa na Tunduru.
“Mkoa wa Ruvuma pia unapata umeme kutoka kwa wawekezaji binafsi wa Kampuni za Tulila na Andoya ambao wana uwezo wa kufua umeme megawati 5.5 na kuingiza kwenye Grid ya Taifa’’,alisema Mwakasege.
Amewataja wateja waliounganishiwa umeme katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 kuwa ni 7,411 ukilinganisha na lengo la mwaka la kuunganisha wateja 6,000 sawa na asilimia 123.