Mfungaji wa magoli matatu wa timu ya soka wasichana ya mkoa wa Mwanza Aaliyah Fikiri (10) akijaribu kumtoka beki wa Arusha Sharifa Mohamed ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Oldean ya karatu Arusha katika mchezo wa nusu fainali ambapo Mwanza ilishinda 6-1.
Patashika katika lango la timu ya soka ya wasichana ya mkoa wa Lindi kufuatia mashambulizi makali kutoka kwa wachezaji wa Tabora ambapo Tabora ilishinda 1-0
*********************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Timu ya soka wasichana kutoka mkoa wa Mwanza ambao ndiyo mabingwa watetezi wa kombe la UMISSETA watakutana na timu machachari ya wasichana kutoka mkoa wa Tabora katika hatua ya fainali alhamis ijayo.
Tabora na Mwanza zinakutana fainali kwa mara nyingine kufuatia timu hizo jana kufanikiwa kuzitoa Lindi na Arusha.
Mwanza ndiyo ilikuwa ya kwanza kuingia fainali baada ya kuibugiza Arusha magoli 6-1 ambapo katika mchezo huo wachezaji wawili wa Mwanza kila mmoja alifunga magoli matatu.
Nyota wa mchezo huo alikuwa ni kiungo mshambuliaji wa Mwanza Sharifa Hamidu huku magoli ya Mwanza yakifungwa na washambuliaji Aaliyah Fikiri na Hadija Petro ambao kila mmoja akifanikiwa kutumbukiza mpira nyavuni mara tatu.
Tabora wao waliingia fainali kwa kuifunga Lindi 1-0, goli lililofungwa na mshambuliaji wao hatari Sozi Juma kufuatia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa baada ya wachezaji wa Lindi kufanya madhambi nje kidogo ya eneo lao la penati.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo wa nusu fainali, kocha wa Arusha Frank Nyange alisema kuwa wachezaji wake walipambana kujaribu kurudisha magoli hayo lakini uzoefu uliwagharimu na akaahidi kufanya vizuri katika mashindano yajayo ya UMISSETA.
Naye Kocha wa Mwanza Michael Otieno alisema kuwa kilichowasaidia wachezaji wake katika mchezo huo ni kubadili mbinu kwa wachezaji wake kucheza pasi fupifupi baada ya kuwasoma Arusha wakitumia pasi ndefu hali iliyochangia kupatikana kumiliki mpira na kupata magoli mengi.
Hata hivyo Otieno ametabiri mchezo mgumu kati ya Mwanza na Tabora kwani timu hizo mbili zimekuwa na desturi ya kukutana mara kwa mara katika michezo hiyo, huku Kocha wa Tabora Mwalimu Ramadhan Idd akitamba kulipiza kisasi kwa Mwanza safari hii.
“Mwanza tunawafahamu na tumejipanga kupambana nao ili kombe la soka wasichana liende Tabora,” alisema Idd
Katika mashindano ya soka wasichana jumla ya mikoa
Timu za Tabora na Mwanza zimewahi kukutana hatua ya fainali mwaka 2018 na robo fainali mwaka mwaka 2019 ambapo Mwanza iliitoa Tabora katika michuano ya UMISSETA na baadaye kufanikiwa kubeba kombe hilo.