Home Mchanganyiko SILINDE – WAKURUGENZI ,MAOFISA ELIMU WANAOKWAMISHA MIRADI NCHINI KUKIONA

SILINDE – WAKURUGENZI ,MAOFISA ELIMU WANAOKWAMISHA MIRADI NCHINI KUKIONA

0
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Mhe. David Ernest Silinde akizungumza na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 502 kutoka Mkoani Tanga, (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu  hao yanayofanyika ADEM Bagamoyo (picha na Mwamvua Mwinyi).
Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt . Siston Masanja akitoa maelezo ya namna ADEM inaendesha mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 502 kutoka Mkoani Tanga, (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu  hao yanayofanyika ADEM Bagamoyo(picha na Mwamvua Mwinyi).
****************************
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, David Ernest Silinde, amewapa salamu wakurugenzi na maofisa elimu kuwa atakayekwamisha miradi ya elimu kukiona.
Akifungua mafunzo ya Uthibiti ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu Wakuu 502 wa Shule zote za Msingi kutoka Mkoani Tanga, yanayofanyika kwa Siku tatu, katika Kampasi ya ADEM Bagamoyo, Silinde alionya Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Elimu kote Nchini, wenye tabia za kuwatisha Walimu Wakuu wasiotoa Ushirikiano wanapotaka kuwaingilia katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuwaomba fedha za Serikali zilizoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa matumizi yao binafsi au kuwaomba fedha za Asilimia kumi maarufu kama ‘teni pasenti’ hali inayopelekea kukwamisha kukamilika kwa miradi hiyo.
“Nitoe onyo kwa Wakurugenzi na Maafisa Elimu kote Nchini, wanaokwamisha utekelezaji wa miradi ya elimu katika Halmashauri zao.
“Aidha kwa kuzembea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na kuifanya kuchelewa ama kuwaomba walimu Wakuu fedha zinapoingizwa katika Akaunti za Shule kwa matumizi yao binafsi na wakati mwingine kulazimisha kupewa fedha za asilimia kumi, kwani haya yote ni uhujumu wa miradi hiyo na fedha za Serikali, hivyo Serikali haitamvumilia yeyote atakayefanya ubadhirifu katika miradi hiyo, na atakayebainika kufanya haya Wizara haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu” Alisema Silinde.
Kazi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na Afisa Elimu wake ni kuhakikisha wanasimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya elimu inayopelekwa katika Shule zilizopo katika Halmashauri zao na si kuihujumu miradi hiyo yenye lengo la kuboresha mazingira ya utoaji elimu katika Halmashauri zao.
Silinde pia aliwataka Walimu Wakuu wanaoshiriki mafunzo hayo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa ndani kuhakikisha wanakwenda kuyatumia katika kusimamia mtaala, kusimamia rasilimali za Shule, kuandaa na kusimamia mpango wa utekelezaji wa maendeleo ya Shule na kuhakikisha kuna mazingira rafiki ya kazi kwani majukumu hayo yanamfanya Mwalimu Mkuu kuwa mdhibiti Ubora wa kwanza wa Shule.
Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Siston Masanja Mgullah alisema, tayari ADEM imeendesha mafunzo hayo kwa kundi la Walimu Wakuu wa Shule za Msingi 8799 Nchi nzima hadi sasa, Maafisa Elimu Taaluma wa Halmashauri 184, na Wathibiti Ubora wa Shule wa Wilaya 183 na Maafisa Elimu Mikoa, Halmasahuri na Maafisa Elimu Taaluma wa Mikoa wapatao 232 .
Na sasa ni ADEM inatoa mafunzo hayo kwa kundi la Walimu Wakuu 502 kutoka Mkoani Tanga na ametanabaisha kwamba mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa GPE – LANESII.
“ ADEM tumeaminiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia  uwezeshaji wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu Nchini, na mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani, tumeifanya kazi hii kwa ufanisi na weledi mkubwa na tunaahidi kuendelea kuifanya kazi hii kwa weledi ili kufikia lengo la Serikali la kuendesha mafunzo haya ambalo ni kuboresha na kuimarisha utoaji wa elimu ya Msingi Nchini” alisema Dkt. Masanja
Mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu Wakuu 502 kutoka Mkoani Tanga yanafanyika kwa siku 03 yakilenga kuwajengea uwezo Walimu Wakuu hao katika kuimarisha eneo la Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani ili kuchagiza uboreshaji wa Sekta ya Elimu Msingi Nchini katika eneo la Ubora wa Mtaala katika kukidhi mahitaji, Uthibiti Ubora wa Shule, Ubora wa ujifunzaji na upimaji mzuri, Mafanikio ya mwanafunzi, Ubora wa Utawala katika Uongozi wa Shule, Ubora wa Mazingira katika kuboresha Ustawi, Kushirikiana na jamii ili kupata Shule bora na Ufuatiliaji na Tathmini ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani.