Picha na Tiganya Vincent
……………………………………………………………………………
NA TIGANYA VINCENT,RS TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka wananchi na wafanyabiashara katika Mnada wa Ipuli kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya virusi vya corona(COVID-19)
Alisema ikiwa nchini jirani zinakabiliwa na tatizo hilo ni vema kila mkazi wa Mkoa wa Tanzania akachukua hatua za kujikinga kama zinavyoshauriwa na wataalamu wa sekta ya afya.
Balozi Dkt. Batilda alitoa kauli hiyo jana alipokuwa katika ziara ya kukagua ukusanyaji wa mapato na hatua zinazochukuliwa kwa wafanyabiashara wa ng’ombe , mbuzi na kondoo katika Mnada wa Ipuli uliopo Manispaa ya Tabora za kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.
Alisema ni lazima kwenye Minada na maeneo yanayokusanya watu wengi kama vile masokoni , Stendi ,mashuleni kukawekwa ndoo za maji tirikia , sabuni ili wanaofanya shughuli hapo waweze kunawa kila wakati.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameiagiza Idara ya Afya ya Manispaa ya Tabora kuhakikisha inajenga vyoo na kuboresha hali ya usafi katika Mnada wa Ipuli ili kulinda afya za watu wanakwenda siku ya Jumamosi kupata nyama choma.
Alisema ya usafi katika Mnada huo hairidhishi na vyoo vilivyopo ni vichache ukilinganisha ya watu wanaokuwepo siku ya Jumamosi.
Aidha Balozi Dkt. Batilda aliwaahidi wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo kutatua matatizo yanayowakabili ikiwemo la baadhi ya watu kuziba njia ya kupeleka ng’ombe mnadani , ukosefu wa majosho, ukosefu wa nyasi za kisasa za kulisha mifugo na ukosefu wa mbegu bora za ng’ombe
Awali mfanyabiashara wa ng’ombe Haruna Mazoea alisema wamelazima kufuata ng’ombe wa mbegu kutoka Biharamulo mkoani Kagera na wengine nchini Rwanda kama njia ya kuboresha ng’ombe wa Tabora.
Alisema aina ya ngo’mbe kutoka Biharamulo wanafaida kwa kuwa ni wakubwa na wanauzwa kuanzia shilingi milioni 1.8 hadi 2 kwa mmoja.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Tabora ni mwendelezo wa ziara ambazo amezipanga za kukutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzitatua ili kujenga Tabora mpya.