NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MWENGE Wa Uhuru ,umezindua mradi wa maji kata ya Muheza,Mjini Kibaha ,Pwani wenye thamani ya milioni 359.5, ambao chanzo chake cha maji ikiwa ni mto Ruvu kupitia DAWASA,huku ukitarajiwa kunufaisha wakazi 2,541.
Mhandisi wa maji halmashauri ya mji huo,Grace Lyimo alimweleza kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa,Mzee Mkongea Ali kuwa ,mradi huo ni mkombozi kwa wakazi hao.
Alisema ,mradi huo ni kati ya miradi iliyopo chini ya programu ya Taifa ya maji na usafi wa mazingira vijijini ambapo ulichelewa kukamilika kutokana na uhaba wa fedha.
Grace alieleza ,ulisanifiwa na kusimamiwa na mhandisi mshauri M/S Netwas (T) Ltd wa Dar es salaam mwaka 2009/2010 ,Halmashauri na jamii ilishirikishwa katika hatua zote za kuibua mradi mpaka usanifu wake.
“Ujenzi ulianza mwaka wa fedha 2013/2014 chini ya mkandarasi M/S Federick company Ltd wa Dar es salaam kwa gharama ya sh.mil 359.577.570 “
Grace alibainisha ,kutokana na uhaba wa fedha kutoka serikali kuu ,mradi huu ulisimama kwa muda wa takriban miaka 2 mwaka 2015/2016 na kuendelea tena na ujenzi mwanzoni mwa mwaka 2017 na kukamilika mwezi agosti 2018.
“Mradi huo ulikuwa na vituo vya jamii vya kuchotea maji Tisa ambavyo vilikabidhiwa kwa uongozi wa watumia maji Muheza kwa ajili ya usimamizi.Hii iliweza kuongeza vituo viwili na kufanya jumla ya vituo vya jamii kuwa 11 na wateja binafsi 240 pamoja na kupeleka maji mtaa jirani wa Lumumba”
“Baada ya mradi kutanuka na maeneo mengine kupata huduma uongozi wa jumuiya ya watumiaji maji uliomba mradi ukabidhiwe DAWASA ili kusaidia huduma kuwa endelevu na kupunguza gharama za huduma ya maji”alifafanua Grace.
Mkongea aliukubali mradi huo na kusema maji ni haki ya kila mtu ,na aliiomba jamii kutunza vyanzo vyake ili miundombinu ya maji iweze kudumu.
Alisema, serikali inatekeleza kauli mbiu ya KUMTUA MAMA NDOO YA MAJI KICHWANI na kutekeleza sera ya maji ya mwaka 2002 ya kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kila upande kwa kila kaya pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.
Awali mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alisema ,mwenge wa Uhuru umepitia miradi 11 ,yenye thamani ya sh .bilioni 2.464.
Assumpter alielezea, mradi mmoja umezinduliwa,mmoja umefunguliwa,miwili imewekwa mawe ya msingi na miradi saba imetembelewa.