Maafisa kutoka Tume ya Utumishi wa Umma wanaadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021 katika Wilaya ya Kisarawe kwa kupokea kero, malalamiko na changamoto za kiutendaji na kuzitafutia ufumbuzi kutoka kwa watumishi wa umma. (Picha na PSC)
***************************
Maafisa Utumishi nchini wametakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na Maelekezo halali yanayotolewa na Serikali wanapotoa ushauri kwa Viongozi na wanaposhughulikia masuala ya kiutumishi kwa watumishi walio chini yao kwa kutoa ufafanuzi wa kisheria wa masuala ya Kiutumishi pale yanapohitajika.
Afisa Rasilimali Watu kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Bibi Saada Ibrahim amesema haya leo Wilayani Kisarawe wakati wa kutoa huduma ya kusikiliza, kutoa ufafanuzi na kutatua changamoto za kiutendaji zinazowakabili watumishi wa umma.
“Baadhi ya Watumishi wa Umma na Wadau wetu waliofika kupatiwa ufafanuzi wamesema kuna umuhimu kwa Maafisa Utumishi kutenga muda sehemu zao za kazi ili kuwaelimisha watumishi masuala ya kiutumishi na suala hili linapaswa kuwa ni endelevu. Kutowaelimisha watumishi wa umma umuhimu wa kufahamu Haki na Wajibu wao, kufahamu vizuri Sheria, Kanuni, Taratibu na Maelekezo halali yanayotolewa na Serikali kunasababisha baadhi ya Watumishi kushindwa kujua Haki zao na wakati mwingine kufanya makosa” amesema bibi Saada Ibrahim.
Kwa upande wake Bwana Amas Mahagala, Afisa Tawala Mwandamizi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma amesema kwa muda ambao Maafisa wa Tume wamekuwepo Kisarawe kutoa huduma kwa wadau inaonyesha baadhi ya Maafisa Utumishi pamoja na kupatiwa nyaraka mbalimbali za Kiutumishi ili wazisome, wazielewe na wawaelimishe watumishi walio chini yao, bado baadhi hawafanyi hivyo. Ni muhimu nyaraka hizo wakazitumia kutoa elimu kwa watumishi kuliko kuzifungia nyaraka hizo kwenye saraka.
“Changamoto nyingi za watumishi zinazotolewa ufafanuzi hapa zingeweza kupatiwa ufumbuzi na Maafisa Utumishi katika Ofisi zao. Miongoni mwa masuala tuliyowaelimisha wadau wetu ni kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma sura ya 298 (marejeo ya mwaka 2019), hususan ufafanuzi wa kubadilishwa kada, masuala ya likizo, uhamisho, OPRAS, kupandishwa cheo pamoja na masuala ya nidhamu, rufaa na malalamiko.” Amesema Bwana Mahagala.
Miongoni wa wadau waliofika Kisarawe na kupata ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi ni Bwana Abdul Ngatila ambaye alitoa maoni yake kuwa Maafisa Utumishi wanapaswa kutambua umuhimu wa kufanya kazi zao kwa weledi na umakini mkubwa kwa sababu wanahusika na maisha ya watumishi, haki na wajibu wa watumishi. Afisa Utumishi asipokuwa makini katika kushughulikia suala la mtumishi husababisha malalamiko pale mtumishi akibaini kuwa hakutendewa haki. Bwana Ngatila alitoa ari kwa Maafisa Utumishi kutimiza wajibu wao huku suala la utunzaji wa kumbukumbu wafahamu nalo kuwa ni jambo la msingi.
Tume ya Utumishi wa Umma, itahitimisha siku ya utoaji huduma kwa watumishi na wadau wake katika Wilaya ya Kisarawe kesho Ijumaa tarehe 18 Juni, 2021 na kuanzia Jumatatu tarehe 21-23 Juni, 2021 Maafisa wa Tume watakutana na wadau katika Ofisi ya Tume iliyopo Mtaa wa Luthuli, Jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Tume ya Utumishi wa Umma.
KISARAWE- PWANI
17 Juni, 2021