WANANCHI wa manispaa ya Iringa wametakiwa kuendelea kufanya usafi na kutunza mazingira yanayowazunguka ili kuenedelea kuuweka mji katika hali ya usafi kama ambavyo umezoeleka na kuepukana na kukumbwa na magonjwa ya milipuko ambayo yanaepukika.
Akizungumza kwenye baraza la madiwani wa manispaa ya Iringa,mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah aliyekuwa amekaimu nafasi ya ukuu wa wilaya ya Iringa,alisema kuwa halmashauri ya manispaa ya Iringa imekuwa ikifanya vizuri mara kwa mara katika swala zima la usafi ambalo limekuwa likiitangaza vizuri halmashauri hiyo.
Alisema kuwa watendaji wa halmashauri hiyo na wananchi wote hawatakiwi kubweteka kwa kusifiwa mara kwa mara mji huo kuwa msafi bali wanatakiwa kuendelea kufanya usafi na kutunza mazingia yao kwa kuwa ndio utamaduni wao.
Abdalah alisema kuwa manispaa ya Iringa ikiendelea kuwa safi ndio inatoa taswiara ya mkoa wa Iringa ulivyo,hivyo kutakiwa kuwe na mikakati ya mara kwa mara ya kuhakikisha usafi unafanyika na kuendelea kuwavutia wananchi na wawekezaji waliopo katika mikoa ambayo haina hadhi kama Iringa.
Alisema kuwa sio usafi tu wanafanya vizuri bali hata kwenye sekta ya Elimu wamekuwa wakifanya vizuri na kuubeba mkoa wa Iringa kwenye ngazi mbalimbali za kitaifa pale matokeo yanapokuwa yanatoka huwa mmkoa unabaki kwenye nafasi za juu katika ufauli wa wanafunzi kutoka Iringa.
Aidha Abdalah aliwapongeza watendaji wa halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kuanzia kwa madiwani,watendaji wa vijiji na kata hadi kwenye chama tawala chama cha mapinduzi(CCM) na ndio nguzo ya mkoa wa Iringa kuendelea kung’ara kitaifa.
Alisema kuwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa umekuwa na mikakati imara na inayotekelezeka katika kukuza na kuleta maendeleo kwa wananchi wake licha kuwa bado wanatakiwa kuhakikisha wanatatua baadhi ya changamoto ambazo zinakwamisha maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) manispaa ya Iringa Said Rubeya alisema kuwa wamekuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na watendaji wa manispaa ya Iringa ndio silaha kuwa ya mafanikio yanayoonekana.
Rubeya aliwataka madiwani wa manispaa ya Iringa kuonyesha utofauti wa kimaendeleo tofauti na baraza lilopita kwa kujituma kubuni miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kutatua kero za wananchi ambazo zimekuwa kikwazo cha kufanya shughuli za kimaendeleo kwa wananchi.
Lakini Rubeya alisema kuwa watendaji wa halmashauri wanatakiwa kujibu vilivyo hoja zote zilizotolewa na CAG ili kuondoa sitofaumu inayopelekea halmashauri ya manispaa ya Iringa kupata hati yenye mashaka jambo ambalo sio zuri kwa maendeleo.
Naye Meya wa halmashauri ya manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kuboresha changamoto zinazowakabili ili kuendelea kuwa kwenye orodha ya juu kabisa ya mini ambayo inaongoza kwa usafi na utunzaji wa mazingira.
alisema kuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na watendaji wote wa halmashauri ya manispaa ya Iringa hivyo kutatua changamoto zinazowakabiri watahakikisha wanazitatua kwa wakati.