Mwanaisha Rajabu Mhandisi Miradi TANROADS mkoa wa Dar es salaam akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Ubungo Interchange leo wakati Wakala hiyo ya Barabara ilipotoa elimu kwa wanancji jinsi ya kutumia Interchange hiyo na kuzingatia alama za usalama barabarani ikiwemo kutunza miundombinu ya barabara hizo za juu kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANROARDS Leila Mhaji.
Mdau wa utunzaji wa Miundombinu ya Barabara Dk. Edes Kimaro akizungumza na waandishi wa habari kwenye Interchange ya Ubungo mkoani Dar es salaam wakati TANROADS ilipotoa elimu ya utunzaji wa miundombinu hiyo kwa wananchi watumiaji barabara hizo.
Mwanaisha Rajabu Mhandisi Miradi TANROADS mkoa wa Dar es salaam akitoa elimu kwa wananchi wanaotumia miundombinu ya barabara za juu Ubungo Inetrchange leo jinsi ya kuzingatia sheria za ysalama barabarani na kutunza miundombinu ya barabara hizo.
Baadhi ya wananchi wakivuka kwenye kivuko cha waenda kwa miguu kwenye Interchange ya Ubungo jijini Dar es salaam leo.
Muonekano wa baadhi ya vipande vya Ubungo Iterchange vinavyoonekana kwa chini.
……………………………………………….
WAKALA wa Barabara Tanzania(TANROAD) umewataka wananchi hususani watumiaji wa makutano ya daraja la ‘Kijazi Interchange’ kuzingatia taratibu sahihi za matumizi ya alama zilizowekwa katika eneo hilo ili kuepukana na ajali.
Rai hiyo imetolewa Dar es Salaam leo na Muhandisi wa miradi ya wakala huyo wa mkoa huo Mwanaisha Rajab wakati wa utoaji wa elimu kwa watumiaji wa barabara pamoja na daraja hilo iliyolenga kuepusha matukio mengi ya ajali zinazojitokeza katika eneo hilo.
Alisema kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi mahali hapo kutoka kwa wananchi wakiwemo madereva, wafanyabiashara, waendesha bodaboda ambayo hupelekea kujitokeza kwa matukio mengi ya ajali sambamba na uharibifu wa miundombinu ya daraja na barabara husika mahali hapo.
“Kujengwa hadi kuzinduliwa kwa mradi wa daraja hili ulilenga kupunguza foleni za magari katika eneo hili, tangu lianze kazi kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi hususani kwa taa za kuongezea magari hivyo kupekelea uharibu wa miundombinu pamoja na matukio ya ajali, elimu hii tumeiandaa mahususi ili kuwaelimisha watumiaji wote kuzingatia sheria” alisema Mwanahisha
Mbali na kutowepo kwa matumizi sahihi ya barabara katika daraja hilo, Mwanahisha alisema pia baadhi ya wananchi wamekuwa wakitembea pembezoni mwa nyaya zilizowekwa maalumu kwa ajili ya watu kuingia chini ya daraja na wengine kuvunja wigo wa nyaya hizo, suala alilosema ni kinyume na taratibu na kuwataka kuachana na tabia hiyo ili kuepuka kuingia katika mkono wa sheria.
“Pamoja na matukio hayo pia kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kufanya mazoezi juu ya daraja hususani nyakati za asubuhi na jioni kwa kupita moja ya barabara ya juu iliyojengwa maalumu kwa ajili ya mabasi ya kasi yatakayopita barabara ya Sam Nujoma, tunawataka wote kuachana na hiyo tabia kwa kuwa barabara hiyo haikujengwa kwa ajili ya matumizi hayo” alisisitiza Msimamizi huyo wa miradi wa Tanroad.
Kawa upande wake mmoja wa wadau wa usalama aliyepo katika eneo hilo la daraja la Kijazi lililopo eneo la Ubungo Edess Kimaro, alisema kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa matumizi ya barabara hiyo na hivyo kuhatarisha usalama wa watumiaji wake wakiwemo watembea kwa miguu.
Alisema kimsingi wanaovunja sheria hizo mara nyingi huwa ni waendesha bodaboda pamoja na baadhi ya waendesha magari ambao hupita bila kuzingatia matumizi sahihi ya taa zilizopo eneo hilo na kusababisha ajali kwa baadhi ya nyakati huku akilitaka jeshi la Polisi kutoa ushirikiano kuwadhibiti watu wenye tabia hiyo.
Kimaro alisisitiza kuwa lengo la kujengwa kwa daraja hilo ni kuharakisha kasi ya maendeleo ya mkoa wa Dar es Salaam kwa kupunguza msongamano wa magari uliokuwa ukijitokeza eneo hilo na kudai ajali nyingi zinazotokea eneo hilo zinasababishwa na uzembe wa makusudi kutoka kwa watumiaji wa barabara hiyo.