**************************

Madereva  wa  malori  yaendayo  safari  ndefu  za mikoani   na nje  ya  nchi   wameliomba  jeshi  la  polisi kikosi  cha  usalama  Barabarani   kuyatafutia   ufumbuzi  mapungufu   yaliyopo  katika barabarani  pindi  wawapo  safarini.

Hayo  yameelezwa  leo  jijini Dar es Salaam  na  baadhi  ya  madereva  wa  malori  wakati  wa  uzinduzi  wa  Kampeni  ya  Safiri  salama  iliyozinduliwa  leo  na  kamanda wa kikosi cha usalama barabarani  nchini Wilbrod  Mutafungwa  uzinduzi   uliofanyika  katika eneo  la Bandari.

Madereva   hao   kupitia  uzinduzi   huo  wamemuomba  Kamanda  Mutafungwa kuwezesha uwepo  wa   utaratibu  wa maeneo  ya  maegesho  ya  malori  kwa ajili  ya  mapumziko   ya  madereva  pindi  wawapo  safarini.

Madereva  hao  akiwemo  Dereva Bigirimana Saidi  wamewaomba  Polisi  wa  usalama  barabarani  kuwa  na  mahusiano  mazuri  na  madereva  huku wakiwaomba  kutoa  elimu  zaidi  badala  ya  kuwaandikia tozo  za  makosa.

Kwa  upande  wake   kamanda  wa  Kikosi  cha  usalama Barabarani  nchini Wilbrod  Mutafungwa  amesema serikali na   jeshi  la polisi   usalama  Barabarani limeandaa  maeneo  maalum  kwa  ajili  ya  ukaguzi  wa  malori  yaendayo  safari ndefu  huku   akisisitiza  na kuwataka   askari wa  usalama  Barabarani kufanya  kazi  kwa  misingi na  taratibu  zilizowekwa.

Kamanda  Mutafungwa  pia  ametumia  nafasi  hiyo  kuwaasa madereva  wa  malori  waendao  safari  ndefu  kutenga  muda  wa  kupumzika ili  kuepuka ajali  za  barabarani  ambapo amefafanua  kuwa   baadhi ya  ajali  husababishwa  na  uchovu  wa madereva.

Aidha  Kamanda  Wilbrod Mutafungwa  amesema  katika  kipindi  cha kuanzia  mwezi Januari mwaka huu 2021  mpaka  Mei 25 ,2021 zimetokea  ajali 81 Tanzania  Bara , Majeruhi wakiwa  ni  66 na watu 47  wamepoteza  maisha kutokana  na ajali za barabarani zilizosababishwa  na sababu  mbalimbali  ikiwomo sababu  za  kibinadamu.