Kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma Bi Aziza Mumba,akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa watoa huduma wa afya yenye lengo la kupunguza matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba yanayofanyika jijini Dodoma.
kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya kati Sonia Henry ,akizungumza wakati wa mafunzo kwa watoa huduma wa afya yenye lengo la kupunguza matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba yanayofanyika jijini Dodoma.
………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) mkoani Dodoma imetoa mafunzo kwa watoa huduma wa afya kwa lengo la kupunguza matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba pia imetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba.
Kauli hiyo imetolewa Leo Mei 20,2021 jijini Dodoma Kaimu katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma Bi Aziza Mumba wakati akifungua mafunzo hayo amesema lengo kubwa la kutoa mafunzo kama hayo ni kuhakikisha kupuguza madhara makubwa juu ya athari za dawa kwa watumiaji.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa watoa huduma za afya hivyo,niipongeze TMDA kanda ya kati kwa kuwezesha mafunzo haya na nina uhakika watakaonufaika na mafuzo haya italeta tija kubwa katika utoaji wa huduma kwa mwananchi “amesema
Kaimu katibu tawala huyo wa mkoa ametoa wito kwa mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.
“Wito wangu ni kwa mamlaka kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa vifaa tiba na dawa tunazotumia mbali matokeo chanya lakini vinaweza kuwa na matokeo hasi ,taarifa ziende kwa haraka ili kudhibiti matumizi ya dawa ambazo zina madhara kwa mwanadamu na suala hili ni pan asana hivyo elimu inahitajika zaidi”amesema.
Aidha amesema kuwa kwa sasa hali sio mbaya hasa kwenye eneo la madhara ambapo , mambo yamekuwa mazuri, kutokana na elimu kuendelea kutolewa kila wakati kwa jamii kuhusiana na utumiaji wa dawa na vifaa tiba katika afya ya mwanadamu.
Kwa upande wake kaimu meneja wa mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya kati Sonia Henry amesema mafunzo hayo dhima yake kubwa ni kuwakumbusha watoa huduma katika majukumu yao ili kuwa makini katika kutoa huduma inayostahili na kulinda afya ya jamii .
“Mafunzo haya yanalenga kutoa elimu kwa watumishi wa sekta ya afya kutoka katika halmashauri mkoa wa Dodoma , kuwakumbusha msingi mkubwa wa utoaji wa taarifa kwani utoaji wa taarifa unasaidia kuokoa maisha ya mwanadamu na mara tupatapo taarifa papo hapo tunachukua hatua katika kumlinda mwananchi ili asidhurike na dawa ama vifaa tiba ambavyo ni hatarishi”amesema.
Aidha,amebainisha kuwa zaidi ya watumishi 30 kutoka kila halmashauri mkoani Dodoma wananufaika na mafunzo hayo katika kuwajengea uwezo .
Mamlaka ya dawa na vifaa tiba ni Taasisi ya serikali iliyopo chini ya wizara ya Afya,Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto yenye jukumu la kudhibiti ubora,usalama na ufanisi wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi ili klinda Afya ya jamii.