Home Biashara BASHE AKUTANA NA WAFANYABIASHARA WA MAHARAGE YA SOYA JIJINI DODOMA

BASHE AKUTANA NA WAFANYABIASHARA WA MAHARAGE YA SOYA JIJINI DODOMA

0

…………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

Wafanyabiashara wa  Maharage ya Soya wamepata  soko la kuuza zao hilo nchini china ambapo uhitaji wa soko hilo ni kubwa kulinganisha na uzalishaji hapa nchini.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Hussein Bashe alipokutana na wafanyabiashara hao leo tarehe 20/5/2021 katika ukumbi wa Morena jijini Dodoma.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuona namna ambavyo nchi itaweza kuchangamkia  fursa ya soko , kuongeza uzalishaji na kukidhi  uhitaji wa soko.

Bashe amesema kuwa wazalishaji wakubwa wa zao la soya duniani ni Marekani, Brazil, Argentina, Paraguay, India na China. Wazalishaji wakubwa barani Afrika ni Afrika Kusini, Nigeria, Zambia, Benin na Malawi.

Kwa upande wa Tanzania Soya hulimwa zaidi katika mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe, Mbeya, Rukwa na Ruvuma.

Pia  Bashe amesema kuwa katika upatikanaji wa mbegu mpaka sasa mbegu zinazokidhi soko la China ni Semeki, Saxon na Signal ambazo zimesajiliwa nchini na  zipo aina nne za TARI Uyole (Uyole Uyole 1, Uyole Soya 2, Uyole Soya3 na Uyole Soya 4).

Aidha, Mhe.Bashe ameeleza bei ya Soya katika soko la dunia kuwa Marekani huuza kwa bei ya shilingi 1,200, China shilingi 3,500, Brazil shilingi 1,200 na Urusi shilingi 1,090.

“Tumepata soko la China kwasababu mazao yetu ni non GMO Crop” alisema Bashe

Hata hivyo Bashe alisema mambo ya msingi ni kukubaliana na bei ya Tanzania ya shilingi 3500 kwa soko la China na kutengeneza mfumo wa mkataba (contract fund) unaoonesha  bei atakayopata mkulima.

Katika kuhakikisha hilo Bashe amewataka wafanyabiashara hao kuwasilisha mahitaji ya mbegu zinazohitajika kupeleka kwa mkulima  ili  ASA waweze kuzalisha mbegu hizo kwaajili ya kukidhi mahitaji kwa msimu ujao.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao Bw. Nyasebwa Chimagu amesema alipokea  maombi ya makampuni 70 yanayotaka kuuza Soya nchini China. Kati ya  makampuni hayo 49 ndiyo yaliyoshinda na kupata kibali cha kuuza soya China kutoka na kukidhi hitaji la soko.

 China  kwa mwaka 2019/2020 walizalisha Soya tani 17.1 na mahitaji ya Soya nchini China ni kiasi cha tani 85 ambapo Tanzania imepata soko la kuuza soya ili kukidhi mahitaji hayo.