Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) pamoja na Naibu Waziri wa Afya kutoka China Mhe. Lin Bin wakiwa wameshikilia dawa ambazo hutengenezwa nchini China mapema leo wakiwa Ikwiriri-Rufiji Mkoani Pwani kuzindua Mradi wa Ushirikiano baina na China na Tanzania katika Kupambana na Ugonjwa wa Malaria Wilayani Rufiji.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (kushoto) akiangalia kinga za ugonjwa wa malaria pamoja na Naibu Waziri wa Afya kutoka China Mhe. Lin Bin leo Ikwiriri-Rufiji Mkoa wa Pwani kabla ya uzinduzi wa mradi wa ushirikiano wa pamoja kati ya China na Tanzania kupambana na ugonjwa wa malaria Wilayani Rufiji.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akipima ugonjwa wa Malaria leo Ikwiriir Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani alipoenda kuzindua Mradi wa Ushirikiano wa pamoja baina ya Tanzania na China wa kupambana na ugonjwa wa malaria Wilayani Rufiji.
Picha ya pamoja Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (wa kati kati mstari wa chini) akiwa na Naibu Waziri wa Afya China Mhe. Lin Bin aliyeongozana na wataalam wake kutoka China pamoja na wataalam na wadau wa sekta ya afya nchini.
****************
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya Malaria
ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama isiyo ya maambukizi ya
Ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya kutoka Uchina Mhe. Lin
Bin alipotembelea Ikwiriri, Rufiji Mkoa wa Pwani katika mradi wa
ushirikiano wa pamoja baina ya China na Tanzania katika kudhibiti
ugonjwa wa malaria huku akiongozana na mwenyeji wake Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu.
“China kuwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kimatafa tutaendelea
kushirikiana kwa pamoja katika kusaidia Tanzania inafikia malengo ya
kutokomeza ugonjwa wa malaria” amesema Mhe. Lin Bin na kuendelea
kusema Ugonjwa wa malaria unatibika na kuzuilika
Waziri Lin Bin amesema kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na China
umeleta manufaa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa
kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo Wilayani Rufiji
kutoka asilimia 25 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 4.9 mwaka 2019.
“Kwa muda wa miaka 60 tumekuwa tukipambana dhidi ya ugonjwa wa
malaria ambao umeathiri zaidi ya watu milioni 30, na tangia mwaka 2017
hakuna taarifa zilizolipotiwa kuhusu ugonjwa wa malaria nchini China”
amesema Mhe. Lin Bin huku akiipongeza Tanzania kwa mikakati mizuri
yenye lengo la kuhakikisha inatokomeza ugonjwa wa malaria.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Tanzania, Mhe. Ummy Mwalimu
ameishuruku Serikali ya China inayoongozwa na Rais Xi Jinping kwa
kuendeleza ushirikiano wa enzi uliopo wa baina ya nchi hizo.
Waziri Ummy amesema kuwa ugonjwa wa malaria bado ni tatizo kubwa
sana nchini Tanzania, huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO)
zikionyesha kuwa asilimia 55 ya vifo vitokanavyo na malaria vinatoka
katika nchini saba za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli tumechukua hatu ambali mbali kwa kushirikiana na wadau
wakiwemo China kupambana na malaria na yapo mafanikio makubwa
ambayo tumeyapata” Amesema Waziri Ummy Mwalimu na kuendelea
“Tumeweza kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria kutoka
asilimia 14.7 mwaka 2015 hadi 7.3 mwaka 2018”.
Amesema kuwa wagonjwa wapya wa malaria wamepungua kwa asilimia
26 kutoka watu 161 katika kila watu 1000 mwaka 2014 hadi kufikia 119
katika kila watu 1000 mwaka 2018 huku vifo vitokanavyo na malaria
vimepungua kwa asilimia 55, kutoka vifo 20 katika watu 1000 mwaka
2014 hadi kufikia vifo 9 kati ya watu 1000 mwaka 2018.
“Serikali ya Tanzania itaendela kuchukua hatua kwa kushirikiana na
wadau wetu wakiwemo Serikali ya China kuhakikisha tunapunguza
kiwango cha maambukizi ya maralia hadi kufikia asilimia 1 ifikapo mwaka
2020” alisema Waziri Ummy Mwalimu.