Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, amesema Jeshi la Magereza linaendelea kuboresha utoaji wa huduma za Afya kwa Wafungwa, Mahabusu na Jamii nzima, kwa kuboresha miundombinu ya utoaji huduma, ununuzi wa dawa na vifaa tiba na uwepo wa wataalamu wa Jeshi zaidi ya 700 nchi nzima.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa Wataalamu wa Afya wa Jeshi la Magereza, CGP Katungu, amewata kutekeleza wajibu kwa ufanisi na uzalendo ili kuboresha huduma za Afya, akieleza kuwa uboreshaji huo utasaidia kupunguza rufaa kwa magonjwa yanayoweza kutibika katika vituo vyetu, hali itakayopelekea kupunguza madeni ya matibabu. 
“Niwatake wataalamu wa Afya mkaboreshe utoaji wa huduma, hiyo itasaidia kupunguza rufaa kwa yale magonjwa ambayo tunaweza kuyatibu katika vituo vyetu na kupunguza madeni ya matibabu ya Wafungwa na Mahabusu” amesema CGP. Katungu 
Aidha, amesema ili kukabiliana na changamoto za kugharamia matibabu ya Wafungwa na Mahabusu, Jeshi kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, limeandaa rasimu ya andiko la matumizi ya bima ya Afya kwa Wafungwa na Mahabusu, ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa rasimu hiyo ipo katika hatua ya mapitio na maboresho.
Pia, CGP. Katungu, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuahidi kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kati ya Jeshi la Magereza jijini Dodoma, na kuiwezesha vifaa ili ianze kutoa huduma, huku akiwataka wataalamu wa Afya wa Jeshi kujisajili katika mabaraza ya kitaaluma na kuhuisha leseni zao, huku akielekeza ununuzi wa dawa na vifaa tiba uendane na bajeti iliyopo.
Kwaupande wake, Kamishna wa Fedha na Mipango, CP. Chacha Bina Jackson, amepongeza ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika Zahanati za Jeshi, huku akiagiza kuendelea kutumika kwa Mfumo wa GOTHOMIS, wakati tukisubiri kuanza rasmi kwa mfumo ulioundwa na wataalamu wetu wa TEHAMA wa TPS e-Hospital Management.
Naye Mkuu wa Sehemu ya Afya Jeshi la Magereza, SACP. Nsajigwa Mwankenja, amesema mafunzo hayo yamesaidia kuwajengea uwezo wataalamu wetu, huku yakijumuisha wataalamu zaidi ya 200 kutoka vituoni.