Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya kuhusu uwezekano wa mvua nyingi kuathiri shughuli za kilimo, usafiri na miundombinu nchini, huku wakulima, wafugaji na wadau wa sekta mbalimbali wakitakiwa kuchukua hatua za tahadhari mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika msimu huu wa mvua.
Akizungumza leo Octoba 23,2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema mvua za msimu katika maeneo mbalimbali nchini zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani, huku mfumo wa hali ya hewa wa El Niño ukiendelea kuwa na mchango katika mwenendo wa mvua hizo hadi karibu Februari.
Amesema tathmini za kisayansi za mamlaka hiyo zinaonesha kuwa mvua nyingi zaidi zinatarajiwa kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu, kuanzia Novemba hadi Januari, ikilinganishwa na kipindi cha Februari hadi Aprili, hali inayohitaji maandalizi ya mapema kutoka kwa wananchi na taasisi zinazohusika na shughuli za kiuchumi.
Dkt. Chang’a amesema katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula, mvua nyingi zinaweza kusababisha maji kutuama mashambani, mafuriko na mmomonyoko wa udongo, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na kuharibu miundombinu inayotumika katika uzalishaji wa chakula.
Ameongeza kuwa unyevu mwingi unaweza kuongeza uwezekano wa kuenea kwa magonjwa ya mazao yanayosababishwa na fangasi na bakteria, hivyo wakulima wametakiwa kuandaa mashamba mapema, kutumia mbinu bora za kilimo, kudhibiti maji kutuama na kuvuna pamoja na kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi ya baadaye.
Katika sekta ya mifugo, amesema mvua hizo zinaweza kuongeza upatikanaji wa maji na malisho, lakini pia kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa kama Homa ya Bonde la Ufa na ugonjwa wa miguu na midomo, hivyo wafugaji wanapaswa kuzingatia mbinu bora za ufugaji na kufuatilia ushauri wa wataalamu.
Amesema sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani nayo inaweza kuathiriwa na mabadiliko ya mazingira ya maji yanayosababishwa na mvua nyingi, ikiwamo kupungua kwa kiwango cha chumvi katika maji ya bahari, hali inayoweza kuathiri uzalishaji wa mwani. Wadau wametakiwa kufuatilia taarifa za utabiri wa kila siku na siku tano zinazotolewa na TMA.
Dkt. Chang’a amesema mvua zinaweza kuwa na manufaa kwa sekta ya utalii na wanyamapori kwa kuongeza upatikanaji wa maji na malisho katika hifadhi, lakini pia zinaweza kuongeza hatari ya kusambaa kwa magonjwa kati ya wanyamapori na mifugo. Alizitaka mamlaka husika kuimarisha miundombinu ya hifadhi na jamii kutoa taarifa mapema wanyamapori wanapoingia katika makazi ya watu.
Aidha ameonya kuwa mvua nyingi zinaweza kuathiri miundombinu ya usafiri, ikiwamo reli ya kisasa ya SGR, barabara, madaraja na shughuli za bandarini, pamoja na kuchelewesha upakiaji na upakuaji wa mizigo na kuathiri usafiri wa anga.
Kutokana na hali hiyo, wadau wa usafirishaji wametakiwa kukagua na kuimarisha miundombinu mara kwa mara ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, huku wakizingatia tahadhari na miongozo inayotolewa na mamlaka husika kuhusu hali ya hewa.
Akizungumzia mwelekeo wa mvua katika maeneo mbalimbali, amesema Kanda ya Magharibi inayojumuisha Kigoma, Tabora na Katavi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, zitakazoanza kati ya wiki ya nne ya Oktoba na wiki ya kwanza ya Novemba na kumalizika kati ya wiki ya nne ya Aprili na wiki ya kwanza ya Mei.
Amesema Nyanda za Juu Kusini Magharibi, zinazojumuisha Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe, pia zinatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, zitakazoanza wiki ya kwanza na ya pili ya Novemba na kumalizika kati ya wiki ya nne ya Aprili na wiki ya kwanza ya Mei.
Kwa upande wa Kanda ya Kati, inayojumuisha Dodoma na Singida, amesema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani, zikianza wiki ya pili na ya tatu ya Novemba na kumalizika kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili.
Ameongeza kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara inatarajiwa kuanza kupata mvua kati ya wiki ya nne ya Oktoba na wiki ya kwanza ya Novemba, huku mvua katika mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Desemba na kumalizika kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili.
Ametoa wito kwa wananchi, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kufuatilia taarifa na miongozo ya TMA na kuitumia kupanga shughuli zao za kila siku, akisisitiza kuwa maandalizi ya mapema na kuzingatia ushauri wa wataalamu ni muhimu katika kulinda maisha, mali na miundombinu dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi.
