Kikao kikiendelea
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati wa kikao chao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akimkaribisha Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam. Waziri Duddridge ameambatana na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar
Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. David Concar (wa kwanza kulia) na baadhi ya maafisa kutoka ubalozi wa Uingereza wakifuatilia kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge
Sehemu ya wakurugenzi na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge (mwenye tai ya bluu) pamoja na Balozi wa Uingereza Mhe. David Concar, Maafisa kutoka Ubalozi wa Uingereza, Wakurugenzi kutoka Wizarani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge wakati wa kikao chao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam
**********************************
Na Mwandishi wetu, Dar
Uingereza imesema Tanzania ni mbia wake muhimu wa miaka mingi katika maendeleo na Jumuiya ya Madola na kuahidi kuwa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kidiplomasia, biashara na uwekezaji.
Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Duddridge ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika mazungumzo rasmi aliyoyafanya na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili
“Lengo la ziara yangu hapa Tanzania ni kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya Uingereza na Tanzania licha ya changamoto ya ugonjwa wa COVID – 19 ambapo Uingereza tumekusudia kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi, mapambano dhidi ya rushwa lakini pia katika sekta za afya na elimu,” amesema Mhe. Duddridge.
Akizungumzia ziara hiyo ya waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema ziara hiyo ni kielelezo cha Tanzania kuheshimika na kukubalika miongoni mwa Jumuiya za Kimataifa na Mataifa ya nje na kwamba kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita ni diplomasia ya uchumi ambapo Uingereza ni moja kati ya nchi tatu kubwa zinazowekeza hapa nchini na hivyo kuwa ni miongoni mwa Mataifa muhimu kwa Tanzania katika kukuza diplomasia ya uchumi.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa katika mazungumzo yao msisitizo mkubwa umewekwa katika uchumi na kukuza biashara pamoja na kuiendeleza miradi mikubwa iliyokuwa ikitekelezwa na Uingereza ikiwemo miradi ya kiwanda cha sukari na madini.
“Ujio wa Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. Duddridge hapa nchini inathibitisha kuwa mahusiano ya Tanzania nje ya mipaka yake bado ni imara licha ya taarifa potofu zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya nje zikitilia mashaka juu ya diplomasia ya Tanzania nje ya nchi,” amesema Balozi Mulamula.
Aidha, kuhusu masuala ya biashara na uwekezaji Balozi Mulamula amemuhakikishia Mhe. Duddridge kuwa mazingira ya uwekezaji ni salama na yanavutia baada ya kuboreshwa na hivyo kumtaka kuwahamasisha wawekezaji kutoka Uingereza kuja hapa nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Mara baada ya mazungumzo na Balozi Mulamula Waziri Duddridge amekutana na Waziri wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Waziri wa Uwekezaji Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Mhe. Geoffrey Mwambe na baadae kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kesho (Jumatano) anatarajia kwenda Zanzibar kukutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kabla ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili hapa nchini.