Home Mchanganyiko WAZIRI MKUU ATAKA WABUNIFU WACHANGA WASAIDIWE,AFUNGA MASHINDANO YA MAKISATU DODOMA

WAZIRI MKUU ATAKA WABUNIFU WACHANGA WASAIDIWE,AFUNGA MASHINDANO YA MAKISATU DODOMA

0

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Joel Ngoko kuhusu mashine ya maji ya kunawa mikono inayojiendesha yenyewe (automatic hand wash machine) katika kilele cha Maonesho ya Mashindano ya Sayansi, Tekinolojia na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 11, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Clinton Joseph kuhusu mashine ya kutengeneza  vifungashio vya karatasi katika kilele cha Maonesho ya Mashindano ya Sayansi, Tekinolojia na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 11, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa tuzo mbalimbali  katika kilele cha Maonesho ya Mashindano ya Sayansi, Tekinolojia na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 11, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kilele cha Maonesho ya Mashindano ya Sayansi, Tekinolojia na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 11, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza katika kilele cha Maonesho ya Mashindano ya Sayansi, Tekinolojia na Ubunifu yaliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 11, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

****************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi na mamlaka ambazo zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga zihakikishe zinawawezesha kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao.

“Taasisi za sayansi na teknolojia; vyuo vikuu; taasisi za utafiti na maendeleo; na mamlaka mbalimbali kama SIDO, VETA na DON BOSCO ambazo kwa namna moja ama nyingine zinashiriki kuendeleza wabunifu wachanga ziwasaidie kubiasharisha ubunifu na uvumbuzi wao,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leoMei 11, 2021 jijini Dodomawakati akifunga maonesho ya Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri.

Amesema kuwa uendelezwaji wa wabunifu na wavumbuzi ufanyike kwa kasi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha matunda ya jitihada zinazofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia za kuwaibua na kuwatambua wabunifu wachanga zinazaa matunda.

“Nitoe wito kwa taasisi zote kutumia ubunifu na uvumbuzi unaozalishwa nchini kama nyenzo muhimu wakati wa kuandaa na kutekeleza mipango mbalimbali inayoandaliwa katika sekta zote, iwe za huduma au uzalishaji, ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo ya Taifa letu” amesema.

Pia amezitaka taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti na maendeleo zishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, hasa ya viwanda, na ziweke utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa nchini na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Nia ya Serikali ni kuona ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia zinazozalishwa na wabunifu wachanga unatoa mchango mkubwa katika kuzalisha ajira mpya, kuongeza kipato kwa wabunifu na kuchangia katika pato la Taifa.” amesisitiza.

 Waziri Mkuu amesema ni vema iandaliwe kwa namna ambayo itawawezesha wahitimu kuwa wabunifu na mwisho wa siku waweze kutumia ubunifu huo kujitengenezea ajira zao wenyewe na ikiwezekana, wawaajiri wengine.

Ameeleza kuwa  kuhusu suala la hatimiliki za wabunifu, Waziri Mkuu amesema anatarajia kuona mabadiliko ya haraka kwenye eneo hilo kwani hadi sasa idadi ya maombi yaliyowasilishwa kutoka Tanzania ni ndogo sana ikilinganishwa na maombi kutoka nchi jirani.

“Takwimu zilizotolewa na Shirika la Hatimiliki Duniani (World Intellectual Property Organization – WIPO) zinazoonesha kwa mwaka 2020, Tanzania iliwasilisha maombi ya hatimiliki nane tu, ikilinganishwa na nchi moja ya jirani iliyowasilisha maombi ya hatimiliki 372; na Afrika Kusini iliyowasilisha maombi ya hatimiliki 1,514. Idadi hii ni ndogo sana, ninatarajia kuona mabadiliko katika eneo hili, haraka sana.”

“COSTECH tumieni nafasi yenu kuwaelimisha wabunifu umuhimu wa kuhakikisha kuwa ubunifu na uvumbuzi wao unatambuliwa na kupewa hatimiliki na hatimaye kubiasharishwa. Elimu kuhusu hakimiliki ni muhimu kwani itawawezesha wabunifu kulinda ubunifu wao. Wekeni mikakati ya kuwaelimisha wabunifu wachanga husasan walioko katika sekta isiyo rasmi kuhusu umuhimu wa kuwa na hakimiliki,” 

Awali Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe.Omar Kipanga amesema kuwa maonesho hayo ni moja ya mkakati wa wizara hiyo wa kuibua wabunifu na kukuza teknolojia miongoni mwa vijana. “Hii tunaamini itasaidia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza fursa kwa wabunifu kujipatia kipato,” alisema.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Godfrey Mulisa amesema kuwa Shirika hilo kwa kushirikiana na COSTECH wameandaa mradi mwingine ujulikanao kama UFUNGUO ambao utazinduliwa Jumatatu ijayo ukiwa na lengo la kuendeleza ubunifu miongoni mwa vijana.

Hata hivyo amewapongeza washiriki wa mashindano hayo kwa kupeleka kazi zao za ubunifu na kuamua kuzishindanisha.