Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa kutoka Wizara ya Maji, Domina Msonge akizungumza wakati wa ufunguzi. Kulia kwake ni Mhandisi Mkuu kutoka Wizara ya Maji, Mhandisi Abdallah Mataka na kushoto kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Maji chini ya Ardhi, Emmanuel Nahozya na Mwakilishi na Afisa Maji Bonde la Ziwa Victoria, Omari Myanza.
Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa kutoka Wizara ya Maji, Domina Msonge (wa pili kushoto waliokaa) katika picha ya pamoja na wataalam wa mabwawa kutoka taasisi mbalimbali (waliosimama nyuma).
Baadhi ya wamiliki wa mabwawa wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Maji wakati wa warsha kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Maji walioshiriki warsha ya Wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa warsha.
Washiriki kutoka Taasisi za mbalimbali za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa katika picha ya pamoja wakati wa warsha.
Waandaaji wa Warsha ya Wadau kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa katika ya pamoja kabla ya kuanza kwa warsha.
……………………………………………………………………………………….
Wadau wa Mabwawa kutoka taasisi za Serikali na Sekta Binafsi wamekutana Jijini Mwanza katika warsha ya siku mbili kuhusu Miongozo ya Usalama wa Mabwawa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha kwa niaba ya Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Mabwawa kutoka Wizara ya Maji, Domina Msonge alisema, warsha imelenga kujadili na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja changamoto zinazoathiri usalama wa mabwabwa.
Alisema warsha hiyo ni fursa ya kipekee kwa washiriki kujifunza na kuongeza ujuzi na uelewa wa masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa mabwawa ili kulinda Rasilimali za Maji.
“Tunao wataalam hapa ambao watatupitisha kwenye masuala mbalimbali ya usalama wa mabwabwa kuanzia sheria, miongozo, masuala ya kitaalam na changamoto tunazokutana nazo kwenye utekelezaji wa majukumu yetu,” alisema Msonge.
Msonge aliwasisitiza washiriki watumie fursa hiyo kujadili kwa kina na kutoa michango yao ya hoja zinazojikita katika kusimamia usalama wa mabwawa.
“Ni matarajio yetu kutakuwa na hoja za ufafanuzi, hoja ya kupeana ujuzi zaidi na mwisho wa siku, Rasilimali za Maji zitakuwa salama na hili ndio lengo makhsus la warsha hii,” alisisitiza Msonge.
Aidha, alipongeza ushirikiano unaotolewa na wadau kwenye suala zima la usalama wa mabwawa kuanzia kwa wamiliki wa mabwawa, wadhibiti na wataalam wa mabwawa.
Warsha hiyo inashirikisha Viongozi kutoka Wizara ya Maji, Wawakilishi kutoka Taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa mabwawa, Wataalam wa Mabwawa (APPs), Wizara na Taasisi zinazomiliki mabwawa, makampuni yanayomiliki mabwawa, Ofisi za Mabonde na Wawezeshaji wa mafunzo.
Warsha hiyo ya Siku Mbili inafanyikia katika ukumbi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria Jijini Mwanza imeanza Mei 11, 2021 na itamalizika hapo kesho Mei 12, 2021.