Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma kwa njia nne (Km112.3) pamoja na eneo utakapojengwa Uwanja wa Ndege wa Msalato hivi karibuni, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso, akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho na wajumbe wa kamati hiyo kuhusu fidia za wananchi wanaopisha ujenzi wa barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma kwa njia nne (Km 112.3) pamoja na Uwanja wa Ndege wa Msalato utakaoanza kujengwa hivi karibuni, jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, akitoa taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kuhusu hatua za ujenzi wa barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma kwa njia nne (Km112.3) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni mara baada ya wananchi kulipwa fidia zao, jijini Dodoma.
******************************
Serikali imesema kuwa itaanza zoezi la ulipaji fidia hivi karibuni kwa wananchi wote waliochukuliwa maeneo yao ili kupisha miradi ya kimkakati ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato na barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma kwa njia nne (Km 112.3).
Aidha imeelezwa kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 12.7 imeshatolewa na kupelekwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa ajili ya fidia za mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma na kiasi cha shilingi Bilioni 14.5 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Msalato.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Msalato na Matumbulu jijini Dodoma, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amesema kuwa fidia hiyo italipwa kwa kuzingatia sheria na kusisitiza kuwa kila anayedai fidia hiyo atalipwa fedha yake yote.
“Leo nimekuja hapa kuwaeleza kuwa msiwe na wasiwasi juu ya fidia zenu, fedha zimepatikana na mtalipwa kwa mujibu wa sheria zote za nchi zilizopo, pia malalamiko yatasikilizwa kwa wale ambao hawataridhika”, amesema Waziri Chamuriho.
Dkt. Chamuriho amewaelezea wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa barabara hiyo itajengwa kwa sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza itahusisha Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Dry Port (Km 52.3) na sehemu ya pili itaanzia Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala (Km 60) na tayari wakandarasi wa ujenzi wa sehemu hizo wameshapatikana.
Amebainisha kuwa miradi hiyo ikikamilika itasaidia kuvutia fursa za uwekezaji na hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa jiji la Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Amewataka wananchi wa maeneo yanayopitiwa na miradi hiyo kutoa ushirikiano ili kurahisisha zoezi la ulipaji fidia kufanyika kama lilivyopangwa ili miradi hiyo ya kimkakati kuanza mapema na kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, ameitaka Wizara kusimamia wakanadarasi hao kikamilifu katika miradi hiyo na kuhakikisha kuwa inakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mikataba iliyowekwa.
Ametoa wito kwa wananchi wanaopitiwa na miradi hiyo kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano kwa makandarasi na kuacha tabia ya kuhujumu miundombinu ili kupelekea miradi kukamilika kwa wakati.
Awali akitoa taarifa kwa Kamati, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko utahusisha pia ujenzi wa miradi mingine inayohusisha jamii moja kwa moja ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya vinne, visima vya maji vinne na magari matano ya kubebea wagonjwa.
Naye Mbunge wa Dodoma Mjini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, ameishukuru Serikali kwa kuamua kuanza utekelezaji wa miradi hiyo hivi karibuni kwani kukamilika kwa miradi hiyo kutapelekea kuchangamsha na kuleta maendeleo katika jiji la Dodoma.
Miradi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya mzunguko ya Dodoma (Km 112.3) kwa njia nne na Uwanja wa Ndege wa Msalato inafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa fedha za mkopo nafuu kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi