Home Biashara TBL PLC YANG’ARA TUZO YA USALAMA MAHALA PA KAZI 2021

TBL PLC YANG’ARA TUZO YA USALAMA MAHALA PA KAZI 2021

0

 Meneja wa Afya kutoka Wakala    wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi, (OSHA) Jerome Materu (wa pili kulia) akimkabidhi Meneja wa kiwanda cha TBL Plc cha Dar es Salaam, Patel Kilovela, tuzo na cheti cha ushindi wa tuzo ya ushindi katika sekta ya viwanda wakati wa wiki ya Usalama na Afya mahali pa kazi, hafla ya kusherekea ushindi huo ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Ilala, wengine pichani ni wafanyakazi wa kiwanda hicho.  

******************************

Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL Plc), imeshinda tuzo  ya Usalama na Afya Mahala pa kazi kwa mwaka huu kwa upande wa sekta ya viwanda.

Tuzo hiyo inayotolewa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa kazi Nchini (OSHA) imetolewa wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani ambayo kitaifa ilifanyika jijini Mwanza na hafla ya kusherekea mafanikio hayo ilifanyika  Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Akiongea kuhusu mafanikio hayo wakati wa kusherekea ushindi huo, Meneja wa Kiwanda cha TBL Plc cha Ilala, Patel Kilovela, amesema ushindi huo umedhihirisha  jinsi ambavyo kampuni inazingatia kanuni za Usalama na Afya mahali pa kazi katika maeneo yake yote ya kazi hususani kwenye viwanda vyake vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha.

Kwa niaba ya kampuni aliwashukuru wafanyakazi wote,wakandarasi  na wadau wote kwa kuunga mkono sera ya kampuni kuhusiana na usalama na kuzitekeleza kwa vitendo, na kuahidi kuwa  kampuni imejiwekea lengo la uhakikisha kanuni za usalama zinatekelezwa ipasavyo katika maeneo yake yote ya kazi kwa viwango vya kimataifa.