Meneja wa Afya kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi, (OSHA) Jerome Materu (wa pili kulia) akimkabidhi Meneja wa kiwanda cha TBL Plc cha Dar es Salaam, Patel Kilovela, tuzo na cheti cha ushindi wa tuzo ya ushindi katika sekta ya viwanda wakati wa wiki ya Usalama na Afya mahali pa kazi, hafla ya kusherekea ushindi huo ilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Ilala, wengine pichani ni wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL Plc), imeshinda tuzo ya Usalama na Afya Mahala pa kazi kwa mwaka huu kwa upande wa sekta ya viwanda.
Tuzo hiyo inayotolewa na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa kazi Nchini (OSHA) imetolewa wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani ambayo kitaifa ilifanyika jijini Mwanza na hafla ya kusherekea mafanikio hayo ilifanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akiongea kuhusu mafanikio hayo wakati wa kusherekea ushindi huo, Meneja wa Kiwanda cha TBL Plc cha Ilala, Patel Kilovela, amesema ushindi huo umedhihirisha jinsi ambavyo kampuni inazingatia kanuni za Usalama na Afya mahali pa kazi katika maeneo yake yote ya kazi hususani kwenye viwanda vyake vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha.