Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati), akiwaongoza watumishi wa wizara yake kuimba wimbo wa mshikamano wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa wizara hiyo (hawapo pichani).Wapili kulia ni Naibu Waziri, Khamis Hamza Chilo.Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akimpongeza Mariamu Salumu kwa kuibuka Mshindi wa Kwanza katika mchezo wa Riadha ya Wanawake ya Mei Mosi iliyomalizika hivi karibuni.Makabidhano hayo yamefanyika leo jijini Dodoma wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa wizara hiyo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akimpongeza Mwanaasha Sungwe kwa kuibuka Mfungaji Bora wa Mpira wa Netiboli katika michezo ya Mei Mosi iliyomalizika hivi karibuni.Makabidhano hayo yamefanyika leo jijini Dodoma wakati wa Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa wizara hiyo.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma (TPS), Dkt. Hortensia Kilonzo akiwasilisha mada kuhusu Maisha baada ya Kustaafu kwa wafanyakazi wa wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi. Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Amani Msuya akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu, Abas Malekela akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (katikati mstari wa mbele),akiwa kwenye picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya Ufunguzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa wizara, Watatu Kushoto ni Naibu Waziri Khamis Hamza Chilo na watatu kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara Christopher Kadio. Kikao hicho kimefanyika leo jijini Dodoma. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
…………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi George Simbachawene amelisisitiza Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo kuzingatia mambo sita ikiwemo mwajiri na mfanyakazi kutambua kuwa sheria za kazi zimetungwa ili kuleta utulivu mahala pa kazi badala ya kuleta migogoro isiyo na tija.
Hayo amesisitiza Leo Mei 7,2021 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa siku moja wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa wizara hiyo jana jijini hapa,Simbachawene alitaja mambo mengine kuwa ni kutoa huduma bila ya upendeleo.
“Jambo la tatu ninalolisisitiza kwenu ni kushirikisha wafanyakazi katika kazi na mipango mbalimbali ya wizara kwa kuzingatia kikamilifu bajeti na mpango wa wizara katika kutekeleza majukumu,”amesema.
Aidha amewataka kuzingatia kanuni za maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma kuwa ni jambo la muhimu na kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.
Simbachawene amesisitiza pia kwa vyama vya wafnayakazi kutumia vyombo vya ushauri ikiwemo baraza la wafanyakazi ili kutatua changamoto mbalimbali katika sehemu za kazi
Hata hivyo Simbachawene amesema wizara ili ziweze kutekeleza majukumu yake ni vyema vyombo hivyo vikashirikiana kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na wizara zinakuwa bora na viwango vinavyokidhi matakwa ya wananchi.
Aidha ametoa wito kwa watumishi kuwa waadilifu na kuendelea kushirikiana na viongozi katika kutekeleza majukumu kwa bidii ili wizara ifike malengo yaliyopangwa pamoja na kuwezesha utekelezaji wa mipango ya kitaifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) wizara ya Mambo ya Ndani John Jembele amesema mkutano huo una lengo la kujadili mwenendo wa wizara kwa kuangalia wapi wamekwama.
“Mkutano huu unafanyika mara mbili kwa mwaka,na tunajadili bajeti yetu ambayo tayari imeshasomwa,tunaiangalia kwa ujumla namna inavyokwenda,na kikao kingine kitakachofuata tutafanya tathimini tumefanya nini katika bajeti tuliyopewa,”amesema
Jembele amesema matarajio yao ni kuona wizara inafanya vizuri na kutoa wito kwa watumishi kufuata na kutekeleza makubaliano ili shughuli za wizara ziende sawa sawa.