Home Mchanganyiko ZOEZI LA UHAMASISHAJI WA UTALII WA NDANI WAZINDULIWA

ZOEZI LA UHAMASISHAJI WA UTALII WA NDANI WAZINDULIWA

0

……………………………………………………………….

Siku ya Jumanne tarehe 04/05/2021, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Monduli, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. ACP Edward Balele pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo ya Monduli Komredi Robert Siyantemi, walishiriki uzinduzi wa zoezi la Uhamasishaji wa Utalii wa ndani.

Tukio hilo lilifanyika kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara. Mwenyeji wa zoezi hilo alikuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Dr Noelia
Myonga.

Moja ya Vivutio muhimu Vilivyotembelewa na Wajumbe hao wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Monduli ni pamoja na Daraja la Kamba linalobembea juu ya miti (canopy/tree top walk way).

Daraja hilo la kipekee kwenye Ukanda wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, lina mzunguko wa mita 400 na sehemu ndefu zaidi kutoka chini (ardhini) kwenda juu ni mita 18.

Wakati huo huo, Wajumbe hao wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Monduli, wamemteua Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli Komredi Robert Siyantemi kuwa Balozi wa Utalii wa Wilaya ya Monduli ambaye atashughulikia mikakati ya kuhamasisha utalii wa ndani ya Wilaya na ule wa nje ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa na ule wa Wilaya ya Monduli.

Vivutio vingine vya Utalii kwenye Hifadhi hiyo ya Taifa ya Ziwa Manyara ni pamoja na Utalii wa kuona Wanyama nyakati za usiku (Night Game Drive); Utalii wa Mitumbwi; Muonekano mzuri wa Bonde la Ufa; Msitu mnene wenye Wanyama wakubwa kama vile tembo, chui, twiga, nyati, pundamilia, nyumbu, swala na simba wapandao miti ambao hawapatikani sehemu yoyote duniani isipokuwa Tanzania.

Vivutio vingine ni pamoja na ndege wazuri kama vile Heroe( (Flamingo) na Korongo domo njano ambao huhama kwenda visiwa vya Comoro na Ushelisheli (Seachells) na kisha kurejea tena kwenye Hifadhi hiyo ya Ziwa Manyara.

Kivutio kingine maarufu ni chemichemi za maji moto ambayo huchemka hadi nyuzi za centigrate 79.